Sunday, 12 October 2014

HAMMO GIZANI: MMEKUWA WANA WA NURU NA WANA WA MCHANA (SURA YA 6)



Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

 

Ewe Muumba na Muumbuaji, twanyenyekea mbele zako tukishukuru kwa yote unayotuwezesha siku baada ya siku. Katika mema au mabaya, Ewe, wabaki kuwa Mungu na Bwana wa maisha yetu na katika yote twakuomba Ewe, Karima utujalie kujua kusudi lako ili tutimize mapenzi yako maishani mwetu siku zote. Kwa hiyo, Mungu Baba, tuzidishie uwepo wako maishani mwetu na utushindanie tunapozidiwa kwa kuwa hatima ya maisha yetu i-mikononi mwako. Amina. 

 

Wapendwa, natumai sote tuwazima na kuwa twazidi kupambanua nyakati tukitumia Neno Takatifu na kwa kumwuliza yeye aliyezifanya nyakati zote kwanzia mwanzo hadi mwisho atufunulie makusudi yake na kutuongoza maishani. Maana, pasi na kufamu Biblia Takatifu pamoja na kujipeana kwake Mola kwa dua, hatutaweza kuimarika kiimani wala kushinda giza inayozidi kugubika mioyo ya wanadamu siku kwa siku. Kumbukeni wale wanawali kumi na jinsi tano kati yao licha ya kujua Neno hawakujitayarisha ipasavyo kumpokea Bwana harusi (Bw. Yesu). Taa (Neno) walizibeba sawa na wenzao lakini hawakutwaa mafuta (Roho Mtakatifu) pamoja na taa zao, ila walitegemea kuwa fahamu zao wenyewe na matendo yao pekee yangetosha kuwafanya wakubalike mbele za Bwana, jambo ambalo Biblia Takatifu yatufunza haliwezekani kamwe. Upambavu wao ni sawa na mtumwa yule aliyepewa talanta (kipawa cha Roho) moja na badala ya kuitumia kama wenzake walivyofanya na kuchuma faida kwa niaba ya Bwana wao, yeye aliamua kuizika na baadaye akamrejeshea Bwana wake ikiwa iyo hiyo moja aliyopewa, (1KOR. 15:50; TIT. 3:5-7). 

 

Na wenzake walipozawadiwa kwa ajili ya wema na uaminifu wao, yeye alikaripiwa kwa ukali na kunyang’anywa ile moja aliyokuwa nayo na kutupwa nje gizani kwenye kilio na kusaga meno. Lakini kabla hayo kumfika, kwanza alijitokeza pamoja na wenzake mbele za Bwana wao mara tu aliporudi toka safari ya siku nyingi nakutaka kufanya hesabu ya mali yake. Hapa nitarudi nyuma kidogo na kuwakumbusheni kuwa Bwana huyu si mwingine ila ni Kristo Yesu mwenyewe, na kama Bwana ni Yesu Kristo kama tulivyoona wiki jana, basi, safari hii ya siku nyingi sio nyingine ila ni kule kuchukuliwa kwake juu mbinguni baada ya kufuka kwake, na kurejea kwake toka huko ndiyo twasubiri, sisi ambao ni watumwa wake (MDO. 1:10-11). Tukirudi kwake yule mtumwa aliyepewa talanta moja, twaona sababu ya kukataliwa kwake ilikuwa ni upambavu aliotenda kwa kumrejeshea Bwana wake talanta ile ile aliyopewa. Fauka ya hayo, alimlaki Bwana wake kwa kumzomea, ati ni mtu mgumu anayevuna asipopanda na kukusanya asipotawanya, yaani, ni kana kwamba mtumwa huyu hana akili razini kumjulisha talanta aliyonayo mkononi nani kampa! Akaongeza kusema, “basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi tazama, unayo iliyo yako.” Matamshi haya yanatufunulia wazi wazi moyo wa mtumwa huyu, jinsi alivyo mdharau Bwana wake na kumchukulia kama mtu asiyefaa lolote.

 

Nitakuulizeni, je, si haki ya mtumwa kumtumikia Bwana wake kwa utimilifu? Na akiwa ni mtumwa mwenye busara, inamfaa kujituma zaidi wakati Bwana wake hayupo ili ahifadhi imani na sifa nzuri alizonazo mbele za Bwana wake. Basi tafakari; itakuwaje baada ya Bwana kuwadhamini watumwa wake kiasi cha kuwagawia mali zake kama mtu afanyavyo na mwanawe na baadaye atakapotaka hesabu ya kazi zao, ajitokeze mmoja kati ya watumwa wale na aanze kumzomea Bwana yule licha ya ukarimu wake na tena kwa dharau amrudishie kile kile alichopewa, huku akidai kuwa Bwana wake huvuna asipopanda! (hukumu nakuachieni). Ila ni dhahiri kuwa mtumwa wa aina hiyo amefarakana kabisa na Bwana wake na wala hakuwezi tena kuwa na maelewano yoyote baina yao. Ama kweli Bwana yule anadhihirisha kusudi la moyo wake kwa kuwapokeza watumwa wale wema na waaminifu mali nyingi zaidi kuliko hapo kwanza na hata kuwakaribisha katika furaha yake. Huku kukaribishwa katika furaha ya Bwana wao sio kwingine ila ni kuwafanya warithi wa mali zake, yaani, wanatolewa utumwani na kufanywa sawa na mwana halisi wa Bwana Yule, kwa kuwa ni mwana pekee ndiye huwa na haki ya kushiriki furaha ya Babake wala sio watumwa, (EBR.1: 1-14).

 

Fika hapa twaona kuwa sawa na wanawali wale wenye busara, watumwa hawa wema na waaminifu wanakaribishwa na Bwana waingie katika furaha yake. Kukaribishwa kule harusini na huku kukaribishwa kwa katika furaha ya Bwana wao ni mamoja. Kwani katika mifano yote miwili; Bwana ni Kristo Yesu na watumwa hawa sawa na wanawali wale ni waumini. Tena katika mifano yote miwili Bwana yule anakawia muda mrefu akiwa mbali; kwenye mfano huu wa Talanta, anachukua siku nyingi safarini, na katika mfano ule wa Wanawali Kumi, anachelewa sana kufika harusini. Vile vile katika mifano yote miwili Bwana anapowasili kuna wale wanaopata kibali na kukubalika mbele zake na kuna wale wanaokataliwa na hata kufukuzwa, na wale aliowakaribisha katika furaha/sherehe yake ni wale waliompendeza kwa kushika maneno yake na kutenda yaliyokubalika wakati wote ule Bwana wao alikuwa mbali nao. Je, mpendwa unajitahidi kutenda matendo yatakayokubalika mbele za Bwana wetu, ili atakaporudi upate kibali mbele zake na akukaribishe katika furaha/sherehe yake, (KOL. 1:9-12). 

 

Tofauti na hao waliokubalika tunaona pia kuna wale waliokataliwa, katika mfano huu wa Talanta ni mtumwa yule aliyepewa talanta moja na kukataa kuitumia talanta ile, sababu ikiwa mtazamo wake duni kwa Bwana wake; ati alimjua kuwa mtu mgumu anayevuna asipopanda! Je, Mkristo mwenzangu mtazamo wako ni upi kuhusu Bwana wetu Yesu Kristo, na kama huna uhakika, (YER. 29:11-13; YN. 10: 7-10). Na kwenye mfano ule wa Wanawali Kumi, sababu ya wale tano wapumbavu kukataliwa ilikuwa ni kutegemea matendo yao licha ya kujua Neno, na kwa mujibu wa Neno hilo kutarajia kuchelewa kwake Bwana harusi ila hawakujitayarisha sawa na lile Neno. Na Bwana harusi alipochelewa (majaribu) kufika walisinzia na kulala (tumaini lao likazima kabisa) hadi waliposikia amewasili ndipo wakaanza kuhangaika jinsi watamlaki. Wanawali hawa wapumbavu sawa na mtumwa huyu walifungiwa nje kwenye giza na huko ndiko kutakuwa na kilio na kusaga meno. Tazama kuwa kule nje si ziwa la moto liko, yaani, hukumu hii inayowafika hawa wapumbavu si ile hukumu ya KIYAMA bali ni hukumu tofauti, hukumu hii ni ile itwayo hukumu ya SIKU YA BWANA, (SEF. 1:14-18; UFU. 6:12-17). Hukumu hii ni ile itakayotekelezwa duniani kote baada ya Kristo Yesu kuwachukuwa watakatifu wake, na kutamatisha kipindi hiki cha Madhila.


No comments:

Post a Comment