Sunday, 5 October 2014

HAMMO GIZANI: MMEKUWA WANA WA NURU NA WANA WA MCHANA (SURA YA 5)



Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.



Ewe, Muumba wa mbingu, dunia na ulimwengu wote, twaliiuna Jina lako tukufu na takatifu lililojaa uweza, na kukushukuru kwa wema na rehema zako maishaini mwetu. Ewe, Mungu uishie milele, twanyeyekea mbele zako tukiomba utujalie uwepo wako maishani mwetu na uweza wako katika yote yanayotukabili. Pia twakuomba utuzidishie rehema zako siku kwa siku kwa kuwa tuwakosaji, viumbe dhaifu ambao msingi wetu ni udongo sawa na fahari yote ya maisha yetu. Ewe, mwingi wa subira, tuongoze kwa neema na utufahamishe njia zako ili tuzipitie siku zote na kwa mwenendo wetu kulifanya Jina lako kutukuzwa na watu wote daima. Amin.



Wapendwa wa Kristo Yesu, kama ilivyo kawaida yetu tukishajipeana kwake Mungu Baba, nakuziendeleza sifa zake twazama katika kuangaza Neno Takatifu ili tuimarishe imani yetu kwa kujifahamisha mapenzi yake Bwana wetu kwetu sisi tunaotumai kumwona ana kwa ana siku isiyo mbali. Mungu Baba kwa mapenzi yake mwenyewe aliridhia kutupatanisha naye tena kwa ukombozi mkuu; ukombozi uliofanyika kwa kifo cha Mwana wake wakipekee Yesu Kristo. Na kwa kumwamini Yesu Kristo twapewa uweza wa kuwa wana wa Mungu, na warithi wa ufalme wake pamoja na Kristo Yesu aliye Mkombozi na Mwokozi wa wote. Yeye ndiye tunasubiri kufunuliwa kwake kama alivyotueleza ili tuwe pamoja naye milele hata milele. Kufunuliwa huku kukaribu mno na inatubidi tujitahidi kulijua Neno lake na kulishika kabisa ili siku itakapofika tusiwe wa kutahayari na kuachwa nyuma kama wale wanawali wapumbavu.



Ni hapo wiki jana tulichambua mfano huu wa wanawali kumi, katika uchambuzi wetu tuliona jinsi Bw. Yesu alivyoutumia kuwaeleza wanafunzi wake kwa mafumbo kuhusu kufunuliwa kwake. Dhamira yake ikiwa kuwapa tumaini la kweli kuwa watamwona tena na kuishi pamoja naye daima milele. Hata sisi tuliopo leo hii tuwashiriki wa tumaini ile sawa na wale waliomsikiliza aliponena mfano huu. Na kwa hakika utakubaliana nami kwamba kwa ukubwa shabaha yake Bw. Yesu alipotabiri kuja kwake kupitia mfano huu, ilikuwa ni sisi Wakristo tuishio katika nyakati hizi za mwisho, sawa na mfano unaoufuata wa Talanta, (MAT. 25:14-30). Mfano huu wa Talanta ndiyo tutaangazia katika somo letu la wiki hii. Na kwa kifupi, mfano huu unatueleza kuhusu Bwana mmoja aliye waita watumwa wake na kuwakabidhi mali zake; kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake, kisha Bwana huyo akafunga safari ya siku nyingi. Halafu muda mrefu ulipokwisha Bwana yule alirejea na kufanya hesabu ya mali aliowapa watumwa wake na kuwazawadia kila mmoja kwa kadri ya bidii yake. Ila tofauti na mfano wa wanawali, baada ya kuumaliza mfano huu Bw. Yesu, aliongeza maelezo yaliyofafanua mafumbo yake. Katika kufafanua mfano huu anaelezea vile Mwana wa Adamu atakavyokusanya mataifa mbele zake na kuwabagua, huku akiwakaribisha wale awaitao kondoo, waurithi ufalme wa Mungu na kuwafukuza wale awaitao mbuzi na kuwatupa katika moto wa milele.



Kabla hatujazama zaidi katika majadala wa leo ni vema kukumbuka kuwa mfano huu wa Talanta ndiyo unatamatisha jibu lake Bw. Yesu alipowajibu wanafunzi wake swali lao walipomwomba awajuze ni nini itakuwa dalili ya kuja kwake na ya mwisho wa dunia. Kwa hiyo, upambanuo wowote wa mfano huu lazima uwiane na maelezo yale mengine ambayo Bwana alitangulia kuwaeleza wanafuzi wake kuhusu ni nini itakuwa dalili ya kuja kwake na ya mwisho wa dunia. Sababu ya kusema hivi ni kuwa mfano huu hutumika visivyo, ususan, kuwatia vijana motisha kutambua talanta zao na kuzitumia kama njia ya kujinasua na umasikini kwa kujitafutia riziki pasi na kutegemea kazi za kuajiriwa. Sisemi kuwa hivi ni vibaya, la, ila nasema kuwa uelewa huo hauwiani na madhumuni yake Bwana wetu, ikizingatiwa swali alilokuwa akijibu aliponena mfano huu.



Natuutazame mfano wenyewe: Mfano unaazia mstari wa kumi na nne kwa maneno, ‘Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri,’ swali la kujiuliza hapa ni, nini hiki ambacho kinafananishwa? Nalo jibu lake twalipata katika aya iyo hiyo katika mstari wa kwanza, ‘Ndipo ufalme wa mbinguni utafanana na,’ kwa mujibu wa mstari huu ni bayana kuwa Bw. Yesu, anaendeleza jibu lake kwa swali la wanafunzi wake na ndiyo maana haoni haja ya kujirudia neno kwa neno anapoanza kuwasimulia mfano huu. Naye mtu huyo atakaye kusafiri si mwingine ila ni Yesu Kristo mwenywe, na hili twajua kwa mujibu wa maelezo yale aliyoyatoa mara tu alipomaliza kusimulia mfano huu wa talanta; mstari wa thelathini na moja. Ila kwa wale watakao ushahidi zaidi kwamba Bw. Yesu ndiye mwana wa Adamu, someni; (MAT. 8:20; 12:6-8; 13:41-43, LK. 19:9-10;). Nao, watumwa wale wanatuashiria sisi tuliookoka kwa kumwamini Bwana Yesu Kristo; hapa najua kuna wale watakaouliza itakuwaje Bwana atufananishe na watumwa? Ee, kwa kweli jambo hili si la kushanganza wala kudunisha kwani hata Mitume walipenda kujitambulisha kama watumwa wa Kristo Yesu hasa Mtume Paulo, (RUM. 1:1). Nazo mali walizopewa kila mtu kadiri ya uweza wake za ashiria vipawa Vya Roho Mtakatifu ambavyo Bwana humgawia kila moja kwa hekima na mapenzi yake, (RUM. 12:1-9).



Japokuwa tushaona kuwa ni Bwana atukirimiaye vipawa kwa hekima na mapenzi yake. Ningependa tutazame mstari wa kumi na tano kwa makini zaidi, “Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.” Kwa mujibu wa mstari huu, kwanza aliwapa mali (vipawa) kisha akasafiri, walakini, kama tujuavyo vipawa vya Roho vilitambulikana baada ya Pentekoste; siku ambayo Roho Mtakatifu alishuka kama ndimi za moto nakutua juu ya vichwa vya Mitume (MDO. 2:1-4). Je, tutasema kuwa Bw. Yesu alikosea ama hakutilia manani maneno yake alipozungumza vile? Tukumbukeni kuwa kile Bw. Yesu anachokifanya hapa ni kutabiri na hata kama ni kwa mafumbo, matukio ya mambo yale yatakapotimia lazima yafuate utaratibu ule. Na kwa kuwa baadhi ya mambo yale yalitimia muda mfupi baadaye, twajua kwa uhakika kuwa yalitendeka sawa na utaratibu wa unabii huu. Kwani kabla ya Pentekoste Bw. Yesu alitangulia kuwabatiza wanafunzi wake kwa Roho Mtakatifu kwa kuwavuvia na kuwaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu,” (YN. 20:22). Basi tutasemaje kuhusu yaliyotukia siku ya Pentekoste! Yaliyotukia siku hiyo ya Pentekoste yalithibitisha aliyokuwa tayari ameyatenda Bwana, (MDO. 1:6-9). Hali kadhalika, lazima kila Neno katika Biblia Takatifu litimie kadiri ya utaratibu wa vile ambavyo Neno lile lilinenwa, isitoshe, hata wewe mpenzi wa Mungu kama alikuahidi jambo subiri tu, maana, lazima litatimia sawa na Neno lake, hata kama matukio yanayokukabili hayaonyeshi dalili yoyote.



Nao watumwa wale walipopokea mgao wao, kila mmoja alifanya kama alivyoona ni vema machoni pake; aliyepokea talanta tano akazifanyisha biashara na kupata faida ya zingine tano na aliyepokea mbili vile vile akapata faida ya zingine mbili, ila, yule aliyepewa talanta moja alichimba shimo nakuizika talanta ile mle dani. Fika hapa wapendwa, ningalipenda kwanza tukumbuke somo la wiki jana, hasa pale tuliposoma kuhusu vipawa vya Roho Mtakatifu, na jinsi mtu aliyepewa kipawa fulani, huwa pia anayomamlaka juu ya kipawa kile. Kisa na maana ikiwa ni tabia ya mtumwa huyu aliyepewa talanta moja na badala yake kuitumia anaamua kuizika katika ardhi hadi Bwana wake atakaporudi ili amrejeshee. Hapa twafahamishwa kuwa kuna baadhi ya waumini watakaobarikiwa na vipawa na kwa makusudi watakataa kutumia vipawa hivyo. Pili nataka tuone hekima ya Bwana yule, yakuwa hakukosea kugawa kiasi kile alichowagawia kila mmoja ya watumwa wake, maanake, kila mtumwa achuma faida kiasi sawa na kiwango alichogawiwa, isipokuwa tu, yule wa talanta moja. Walakini nasisitiza kuwa huyo mtumwa aliyepewa talanta moja, kwa upumbavu wake, yeye zaidi ya wenzake ndiye anadhihirisha kuwa Bwana wao aliwajua watumwa wake vema, yaani, sio uweza wao tu bali hata udhaifu wao pia aliujua na hili ndilo lamfanya kuwagawiya mali vile.



Naye Bwana yule aliporudi toka safarini akaja kufanya hesabu ya mali yake, na watumwa wale wawili wa kwanza wakajitokeza na kuthibitisha wema na uaminifu wao kwa Bwana wao kwa kumletea faida yote waliotengeza. Hapa najua baadhi yetu watajiuliza mbona Bwana anakubali faida ilhali wiki jana tulisoma kuhusu wale wauza mafuta (makuhani/ wachungaji) ambao Bwana mwenyewe aliwaita manabii wa uongo. Makuhani wao hao aliwafananisha na mbwa mwitu wakali wanaovalia ngozi ya kondoo, sababu ikiwa ni tamaa yao ya fedha na kwa ajili ya tamaa iyo hiyo wanapofika mbele zake anawakemea na kuwakana kabisa! Ni kweli jambo hili laweza kukanganya kidogo, lakini, ukitizama mifano yote miwili kwa makini hautapata shida kutofautisha kati ya faida ya wale wauza mafuta na ya hawa watumwa. Tofauti kati yao yadhihirika hivi; wale wauza mafuta walikuwa wakijitafutia faida yao wenyewe, hata usiku ule Bwana harusi alipokuja hawakujitokeza kwenda kumlaki. Ilhali, hawa watumwa wanajitokeza mbele za Bwana wao pindi tu anapowasili nakumpa faida yote waliochuma, maanake, kujituma kwao kuliwa kwa lengo moja na lengo hilo lilikuwa kumfurahisha Bwana wao kwa vyovyote vile ili atakapokuja wapate kukubalika mbele zake, (2KOR. 5:4-10).

No comments:

Post a Comment