Monday, 29 September 2014

HAMMO GIZANI: MMEKUWA WANA WA NURU NA WANA WA MCHANA (SURA YA 4)




Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.



Mungu Baba, tunakushukuru kwa ajili ya wokozi na ukombozi uliotufanyia kwa kifo cha Mwanao wa kipekee, Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye ndiye mtangulizi wa vyote na katika yeye vyote viliumbwa iwe, mamlaka, enzi, au usultani, vyote viliumbwa katika, yeye. Ewe, Bwana wetu tunakuhimidi kwa kutufanya wana wa Mungu kwa kifo chako msalabani na kwa kufufuka kwako ukawa malimbuko ya ufufuo na kutufanya tuwe mwili wako kwa uweza wa Roho wako Mtakatifu. Ewe, Kichwa cha Kanisa, uliyetukomboa kwa gharama ya uhai wako twaomba ututakase tena kwa Neno lako Takatifu na utujaze upya kwa Roho Mtakatifu, ili tukaweze imarika katika imani na kuenenda kwa uaminifu na utiifu tukizifuata nyayo zako siku zote za maisha yetu. Amin.  



Wakristo wenzagu, kama ilivyo kawaida yetu baada ya dua na kumtukuza Mungu, hufuata marudio ya yale tuliyosoma Juma lililopita kwa kifupi. Kwenye Somo la Juma lililopita tulitilia manani umuhimu wa ubatizo kwa Roho Mtakatifu, na mwongozo tulioufuata ulitokana na jibu lake Kichwa cha Kanisa kwa wanafunzi wake. Wanafunzi walimwuliza Bw. Yesu, ni nini itakuwa dalili ya kuja kwake na ya mwisho wa dunia? Naye alitabiri na kuwaeleza mambo mengi yatakayotukia nyakati za mwisho, na katika jumla ya maelezo yake akawasimulia mfano ule wa wanawali kumi. Mfano huu tuliuchambua kwa kina na kuona jinsi Kristo Yesu alivyonena kwa mafumbo akieleza jinsi kuja kwake kutakavyo kuwa na nini hasa ya wapasa watakatifu wake kufanya ili wakapate kukubalika kuingia mbinguni pamoja naye, huko atakuwa tayari ameandaa karamu.



Basi bila kusita wala kulegeza mwendo tutamalizia kuchambua mfano huo kwa kuangazia wauza mafuta. Kumbukeni kuwa pale mwishoni mwa somo letu la wiki jana nilidokeza kuhusu wauza mafuta na kusema kuwa wanaashiria makuhani/watumishi wa Mungu! Lakini kwanza hebu turejelee jinsi ujio wa bwana harusi utakavyokuwa, (MAT. 25:5-6): “Hata bwana harusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. Lakini usiku wa manane, pakawa na elele. Haya bwana harusi; tokeni mwende kumlaki.” Kipengee hiki cha tujulisha kuwa mwito ulitolewa kuwaamsha na kuwafahamisha wale wanawali waende kumlaki bwana harusi maana alikuwa ameshawasili. Mwito huu ama sauti hii itakuwa ya malaika mkuu atakayemtangulia BWANA kwa parapanda ya Mungu ili kuwajulisha watakatifu wake watoke kwenda kumlaki, (1THE. 4:15-17). Walakini kama tulivyoona kuna baadhi ya Wakristo ambao hawataruhusiwa kuingia harusini, Sawa na wanawali wale tano wapumbavu waliopatikana kama hawajajitayarisha ipasavyo. Ikawa, badala yao kwenda kumlaki bwana harusi alipowasili iliwabidi watoke usiku huo wa manane kwenda kusaka wauza mafuta ili wauziwe mafuta ya kuwasha taa zao. Ila waliporudi harusini waliupata mlango ukiwa umefungwa, isitoshe, walipodai kufunguliwa, bwana harusi aliwakomesha kwa kuwaambia, hawajui!



Tamko sawa na hili la bwana harusi ambaye tulimtambua kuwa ni Bw. Yesu Kristo, la patikana (MAT. 7:23). Katika aya hii ya saba ukianzia pale mwanzo, Kristo anafunza kuhusu unafiki na kufikia msatari wa 15-20, anautahadharisha hadhira uwe macho kwa ajili ya wale awaitao manabii wa uongo. Fika hapa najua kuna wale watakaotuhumu kuwa nimeanza kupotosha mada tunayozungumzia. Nami nitakuulizeni, kama Kristo Yesu ndiye abatizaye kwa Roho, naye amefunga milango, je, hao wauza mafuta waliobaki nje sawa na wale wanawali wapumbavu wanafanya biashara halali? Tushikilie hapo kwanza huku tukirejelea yale Kristo Yesu anaeleza kuwahusu hao manabii wa uongo, anasema, “tutawatambua kwa matendo yao.” Kisha anafululiza kufafanua anachomanisha ili wewe na mimi pia tukaweze kufaidika kwa kuwatambua na kuwaepuka kwa mapema. Ila cha kushangaza nikuwa anamalizia kwa kusema watamjia siku ile na kusema; Bwana, Bwana, hatukufanya unabii, kufukuza mapepo na hata kutenda miujiza mingi, kwa Jina lako. Naye atawakemea na kuwafukuza watoke mbele zake licha ya shuhuda zao ambazo Bwana hakanushi! Hii ina maana kuwa zile shuhuda ni za kweli. Lakini Bwana haridhii kuwakubali licha ya makuu waliotenda kwa uweza wa Jina lake!



Wapendwa, mbona Kristo anawageuka na kuwakemea watumishi wake? Kweli yeye mwenye haki anaweza kuwahukumu watu wake vile? Kwa kweli hapa kuna wale watakaosema, “Hukumu aliyoitoa Bwana wetu si ya haki kamwe.” Walakini, ni nani mwenye ufahamu wa mambo yote, hata yale ya siri adhaniyo mtu moyoni mwake, je, si yeye yule mwenye haki. Hebu tufanye tendo la busara na kuchunguza hukumu hii anayoitoa Bwana kwa watu waliofanya maajabu makuu kwa uweza wa Jina lake kwa kutumia Maandiko Matakatifu. Bw. Yesu, alitutahadharisha kuhusu manabii wa uwongo aliowataja kuwa mbwa mwitu wakali waliovalia ngozi ya kondoo na hata shuhuda zao zitadhihirisha uweza wa Roho Mtakatifu katika huduma watakazo toa. Kwa mujibu wa maelezo yake Bw. Yesu haitakuwa rahisi kuwatambua manabii wa uongo, kwa kuwa watakuwa wamevalia ngozi ya kondoo na hivyo ukiwatazama kwa macho watafanana kondoo, isitoshe, watakuwa na vipawa vya Roho maana watanena kwa unabii, watawafukuza mapepo na kutenda miujiza si haba. Swali la kujiuliza hapa ni, kama wanatenda haya yote kwa uweza wa Roho, dosari liko wapi hata wakataliwe na Bwana waliyemtumikia?



Mtume Paulo katika waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho, anatujulisha kuwa roho wa unabii humtii nabii, (1KOR. 14:32-33). Hii inamaana kuwa Mungu humpa mtu kipawa, naye aliyekirimiwa kipawa kile ana mamlaka juu ya kipawa alichopewa na jinsi atakavyo kitumia. Naye Mtume Petro, ambaye alikuwa mmoja katika hadhira ile Kristo Yesu alipozungumza kuhusu manabii wa uongo, katika waraka wake wa pili anatuonya vile vile; tujihadhari na manabii wa uongo, (2 PET. 2:1-22). Mt. Petro katika maelezo yake anamtaja Balaamu mwana wa Beori na jinsi alivyo karipiwa na Punda kwa ajili ya uhalifu wake, (2 PET. 2:14-17). Balaamu kwa kweli alikuwa na kipawa cha unabii, yaani, alikuwa mtu aliye zungumziwa na Mungu moja kwa moja, na utabiri wake ulikuwa wa kuaminika, (HES. 22-24). Ila, sawa na hao wanaomjia Bwana na kumweleza mambo makuu waliyoyatenda kwa Jina lake, hakumridhisha Mungu aliyempa kipawa kile, kwa kuwa matendo yake Balaamu hayakuambatana na makusudi ya Mungu juu ya watu wake Israeli, aliolipwa kuwaroga. Ni uhalifu uo huo wa Balaamu, wakupenda fedha unaoangaziwa na KristoYesu katika mfano wa wanawali kumi, maana, Bw. Yesu ndiye hutubatiza kwa Roho Mtakatifu bure na kutugawia vipawa kwa mapenzi yake, (RUM. 5:1-5; 12: 6-9). Kwa hivyo yeyote auzaye mafuta ameanguka katika uhalifu wa Balaamu kwa kutafuta ujira wa udhalimu, (MDO. 8:14-21; YUD. 11).



Wapenzi wa Mungu, la muhimu ni kujua jinsi ya kuwatambua kwa uhakika hawa manabii wa uongo ili tuwaepuke na hukumu yao itakapowajia isitupate sisi pamoja nao, (ISA. 24:1-3). Kumbukeni kuwa Kristo, alianza kwa kutueleza tusihukumu ili nasi tusihukumiwe, hivi nikusema, huwezi mrekebisha nduguyo ilhali wewe uko hatiani. Ujirekebishe kwanza ili ukaweze kumrekebisha mwenzio, lau sivyo, uyatendayo ni sawa na unafiki, maana wewe mwenye hatia kubwa zaidi (boriti) wajiona bora kuliko nduguyo mwenye kosa ndogo (kibanzi) kukuliko, (MAT. 7:1-5). Ila, tukijihukumu kwanza na kujirekebisha kweli kweli kwa kutoa boriti jichoni mwetu na hapo ndipo tutaweza kuona vema na kuweza kukitoa kibanzi jichoni mwa ndugu zetu na wala hapatakuwa na wakutuhukumu, (1KOR. 11:31).


No comments:

Post a Comment