HAMMO GIZANI: MMEKUWA WANA WA NURU NA WANA WA MCHANA (SURA YA 1)
Neema na iwe kwenu na amani,
zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
Wapenzi na ndugu katika Kristo
Yesu, tuliinue jina lake Muumba wa vyote kwa wingi wa karama zake maishani mwetu,
hususan, sisi aliyotuzaa kwa asili ya Roho na moto. Kwa Roho Mtakatifu
ametufanya upya; watu wasioongozwa na tamaa za mwili ambazo huishia mauti, bali
watu wanaoongozwa kwa nia ya Roho ambayo huishia uzimani. Ametufanyia na amani
katika Kristo Yesu, utimilifu wake Mwenyezi, Mungu Baba, asiyeonekana kwa macho.
Tuzidishie Ewe, BWANA wetu wema na rehema zako ili tuijue na kuishika njia yako kwa uhakika, tukikutazamia kufunuliwa kwako. Amin.
Watakatifu kwa Neema ya Kristo
Yesu, hadi sasa sidhani kama kuna ye yote ambaye tumeacha nyuma kuhusiana na mchakato
mzima wa ‘Vipindi Saba Vya Neno La Mungu.’ Tumejadili mambo kadha wa kadha chini
ya kichwa hiki kwa muda unaozidi majuma manne hadi sasa. Utaratibu huo
umetuwezesha kuweka msingi thabiti wakutuwezesha kusoma na kuelewa chuo cha Ufunuo wa
Yohana. Kitabu ambacho kinaogopwa na wengi nakutazamwa kama fumbo kubwa
lisiloweza kufumbuliwa, hivi kwamba wengi wetu hatushughuliki kukisoma kabisa!
Muda wake umetimia, kwa kuwa yaliyoandikwa kwa mafumbo enzi za kale Bwana ameyaweka wazi zamani hizi. Hebu nikuulizeni, enyi wateule zake Mungu Baba, ni Neno lipi, hata moja litokalo kinywani
mwa Baba lafaa kukupita? kama jibu ni hakuna hata moja. Basi tujibidiisheni kukisoma, maana, aliyotaka tuyajue ameyaweka wazi, na zaidi anatuhimiza
kulijua na kulitenda Neno lake. Sadfa na hayo, katika utangulizi wa chuo cha
Ufunuo wa Yohana, baraka spesheli imeahidiwa ye yote awaye Yule atakaye soma na
kuyashika yaliyoandikwa humo, (UFU. 1:3).
Nafanya kurudia: fika hapa tumekuwa tukiangazia
historia nzima ya ulimwengu tangu mwanzo hadi mwisho; Siku ya Kwanza hadi Siku
ya Saba. Kati ya siku hizi, Siku ya Tano ndiyo tuliyoishughulikia kwa kina,
maana, tulitambua siku hii ndiyo tuiishio kwa wakati huu. Kwa hiyo hatuna budi
kuifahamu ili tusiishi sawa na watu wa mataifa pasi na kutathimini yanayotukia
kila uchao au baadaye matokeo yatakuwa ya namna gani. Kama wenye hekima ya kweli kati
ya wanadamu inatupasa zaidi sisi Wakristo kuwa macho na kufahamu vema zamani
hizi tuiishio. Tukizingatia kuwa tunaabudu Mungu wa-kweli ambaye Yeye pekee
anafahamu mambo yote kwa utimilifu; yaliyopita, yanayotendeka, na yatakayotokea,
(ISA. 44:6-8).
Isitoshe, Mungu Baba katika Kisto
Yesu ameipa Kanisa lake karama ya unabii, ili kuhami na mapema aila yake kabla
hajatenda lolote. kwa kuwa kwanza huwajuza manabii zake alichoazimia kutenda nao hutueleza kuhusu
makusudio ya Mola wetu, (UFU. 22: 6-7). Wala si hayo tu, Roho wa Mungu huchunguza
yaliyomo moyoni mwa Mungu Baba na kuwajuza wateule zake, yaani, mimi na wewe
ndugu katika Kristo. Sababu ikiwa kutuwezesha kuishi kwa utakatifu kama watu wa Mungu, ili tusifikwe na
mambo kama watu wasio na ufahamu au hekima, (1KOR. 2:6-16).
Basi Wakristo, njia siyo nyingine ila, ile
ile, walioipitia ndugu zetu walio tutangulia akina; Musa, Yusufu, Daudi, Danieli,
Ezra, Petro, Mathayo, Yohana, Paulo, na juu ya wote Bw. Yesu, Mwokozi na
Mkombozi wetu sote. Yeye alituonesha kwa matendo mfano uliobora zaidi ya wote. Na
mfano huu ndio desturi ya Mwili wake (Kanisa) kote kote duniani na katika
historia na tamaduni za watakatifu wa Mungu. Desturi na tamaduni
hii sio nyengine ila kuomba bila kukoma na kuenda katika utakatifu
tukimtumainia Mungu kwa imani, daima.
Tukitimiza haya sawa na ndugu zetu
kabla yetu, Mungu atatuzidishia karama zote za rohoni na kamwe hatutapungukiwa
kwa lolote. Utiifu wetu kwa Neno Takatifu na kwa dua zetu mbele zake, hizi ndizo zana
walizotumia wenzetu kabla yetu kwa mafanikio makuu na ndizo baado tunazohitaji katika kipindi hiki kilichojaa giza na maovu ya kila aina.
Tusikate tamaa wapenzi wa Mungu maana Mungu ni upendo na hakuna ajuae kupenda
zaidi yake, wala hakuna aliye na uwezo wakupigania wapenzi wake zaidi yake
Mwenyezi, Bwana wa Majeshi, (ISA. 41:1-16).
Tuseme nini zaidi wapenzi wa Mungu?
Mie sioni lingine ila kijibidiisha katika Kulijua Neno Takatifu na kulitenda.
Sawa na ushauri wa Mtume Paulo (1THES. 5:1-11), tukilijua Neno Takatifu tusilale
usingizi kama wengine, bali tujivike kifuani imani na upendo na chapeo yetu iwe
tumaini la wokovu. Kwa kuwa Mungu hakutuweka kwa hasira yake, bali tupate
wokovu kwa Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye alikufa kwa ajili yetu ili tuishi
pamoja naye. Je, mwaona jinsi Mungu Baba alivyotufanya wandani wake? Basi
tusijipunguzie karama iwayo yoyote ile. Tuzidi kutia bidii katika kumlingania
Mungu Baba na kulisoma Neno Takatifu, maana, katika haya atatufunulia yote
aliyotabiri kwa vinywa vya watakatifu wake na kutuandikia katika Biblia
Takatifu.
No comments:
Post a Comment