HAMMO GIZANI: MMEKUWA WANA WA NURU NA WANA WA MCHANA (SURA YA 3)
Neema
na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
Mungu Baba, Ewe, Muumba na
Muumbuaji, twakuabudu na kunyenyekea mbele zako kwa ajili ya ukuu na uweza wako
maishani mwetu. Tukikushukuru kwa yote unayotutendea, Ewe, usiye na hila wala
uovu ndani yako, Baba mwema, unayetufahamisha makusudi yako kabla huja tenda
jambo lolote. Daima mkweli na daima mwaminifu, Jalali, tuzidishie uwepo wako
siku kwa siku ili tuweze kuukabili ulimwengu na maovu yake yote na zaidi tukaweze
kukujua vema na kutembea nawe kwa imani hadidi tukiufuata uelekezi wako, Ewe, mchungaji
mwema wa maisha yetu. Amin.
Wapenzi wa Mungu, enyi manukato
yake Kristo Yesu, utimilifu wake Mungu Baba nawasabahi na kuwakaribisha katika
somo la leo. Shabaha letu likiwa lile lile, kuzidi kujifunza Neno Takatifu la
Mungu Baba yetu. Kama ilivyo desturi yetu, kwanza tutajikumbusha kwa kifupi
yale tuliyosoma wiki jana; tulisoma kuhusu aliyekuwa Mfalme wa Yuda kwa jina
Yosiah, na jinsi alivyotumika na Mungu kuwarejesha watu wake katika imani na
ibada ya kweli. Kadhalika tuliona jinsi Mungu Baba alivyoahidi kumimina Roho
wake kwa wote wenye mwili katika nyakati hizi za mwisho na kuwa atamuinua mtu
atakaye tumika kama Mfalme Yosia alivyotumika, ili awatayarishe watakatifu wa
Mungu wakaweze kumpokea Roho Mtakatifu atakapomiminwa. Jambo la msingi likiwa
kuwawezesha watakatifu kujihami kiroho na kuimarika kiimani ili wakaweze kustahimili
wakati mgumu utakaoifika dunia nzima sawa na Neno la Mungu wa Israeli alilozungumza
kupitia vinywa vya manabii wake.
Somo la leo la ng’oa nanga kwa kuufuata
mkondo ule tulioushika wiki jana na kuendelea kuchunguza umuhimu wa Roho
Mtakatifu kumiminwa juu ya wote wenye mwili katika siku hizi za mwisho.
Mwongozo wetu tunautoa toka mfano ule wa wanawali kumi, (MAT. 25: 1-13). Lakini,
kabla ya kuuchambua mfano huu ni vema tuelewe kiini chake, yaani mbona Bw. Yesu
akafunza vile na kusudi lake lilikuwa lipi kwa wasikilizaji wake. Ukirudi nyuma
kidogo aya ya 24, hapo ndipo funzo nzima la anzia. Bw. Yesu atoka hekaluni na kuukwea
mlima wa mizeituni ili apumzike, huku wanafunzi wake wakimwonyesha utukufu na
ustadi wa Hekalu. Bali Bw. Yesu akawazungumzia na kubashiri yatakayojiri kwa
muda usio mrefu, nao wakamwendea kwa faragha na kumuuliza awaeleze lini mambo
hayo yote yatatendeka na nini dalili ya kuja kwake na ya mwisho wa dunia. Jibu
alilowapa na maelezo yake yakajumuisha matukio mbali mbali yatakayo tendeka
duniani kote katika nyakati za mwisho na akazidisha hata kuwanenea kwa mifano;
mfano huu wa wanawali kumi na hata ule unaoufuata wa talanta ni katika jumla ya
maelezo yake Kristo Yesu. Hata hivyo hatutashughulika na mfano huo wa talanta
kwa sasa, lakini ifahamike kuwa sijamzuia mtu ye yote kujizulia baraka toka
mfano huo, kwani Neno la Mungu liwazi kwetu sote.
Bila pingamizi, mfano huu wa wanawali kumi, q Bw. Yesu aliunena ukiwa mojawapo kati ya maelezo
yake alipolijibu lile swali aliloulizwa na wanafunzi wake kuhusu, nini dalili
ya kuja kwake na ya mwisho wa dunia. Kwa
mukhutasari, katika mfano huu wa wanawali kumi, anaufananisha Ufalme wa
mbinguni na sherehe ya harusi ambayo ikishaandaliwa bwana harusi akakawia
kufika mpaka giza likaingia akiwa baado hajafika na hata waliokuwa wamejiweka
tayari kumlaki wakalala. Cha muhimu ni kuwa sherehe haikuvunjwa na ijapokuwa
bwana harusi alichelewa hatimaye aliwasili kukiwa usiku wa manane na kulakiwa
na baadhi ya waliostahili kumlaki. Sababu ikiwa sio wote waliokuja harusini walikuwa
wamejitayarisha vilivyo kwa sherehe, ilhali kwa kuzibeba taa zao yaonekana wote
walikusudia kuwa bwana harusi angekawia kufika na hata kuchelewa hadi usiku
umpate angali hajafika.
Fika hapa, nadhani ni wazi kwetu
sote kuwa Bw. Yesu anaelezea mambo yaliyo nyeti sana tena kwa mafumbo, dhamira
yake ikiwa ni kuwafunulia mambo yaliyositirika katika Roho wa Mungu kwa njia
watakayoelewa kwa urahisi. Hivi ni kumaanisha kwamba, jibu alilowapa wandani
wake na maelezo yale yaliwahusu moja kwa moja, kwani toka kwao Kanisa (Mwili wa
Kristo), lilipata mafundisho yake Kristo; ambayo ndiyo msingi wa ibada, itikadi
na kanuni za Ukristo. Msingi wa imani ya Ukristo ni kuwa tumaini tulionayo
katika ukombozi wake Kristo Yesu utatimilika atakaporudi kuwachukuwa wote waliowake
toka duniani na kuwapeleka mbinguni halafu ataihukumu dunia. Pasi na tumaini
hii kuwepo katika imani ya Mkristo, bila shaka imani ile imepungukiwa, kwa kuwa
imepuuza ushahidi mzima wa kufa na kufufuka kwake Mkombozi wetu Yesu Kristo.
Maana, katika kifo na kufufuka kwake Mkombozi wetu alitimiza kazi yake ya
kuukomboa ulimwengu na kuupatanisha na Mungu Baba na baada ya kufufuka alijidhihirisha
kwa wanafunzi wake kisha akapaa juu mbinguni kwa ahadi kuwa atarudi tena (kama
mwizi) kuwachukuwa wote waliowake ili wawe pamoja naye mahali alipo.
Mfano huu wa wanawali kumi, haswa,
unaelezea ujio huu wa Bw. Yesu kama mwizi na jinsi watakatifu wake wanavyostahili
kumsubiri yeye bwana harusi wakiwa wamejiandaa vilivyo, kwa kuwa ameandaa
sherehe na hataghairi bali atakuja, hata kama atachelewa na kufika usiku
katikati kwenye giza kuu lazima atakuja. Fika hapa ningependa tutilie maanani
wanawali wale kumi. Tayari tumeona wanaashiria watakatifu wote wamwaminio
KristoYesu, yaani, Kanisa, na ndio maana tunajulishwa kuhusu unawali/ubikra wao.
Kwa hiyo hakuna sababu maalum yakutofautisha kati ya wale tano wenye busara na
wale tano wapumbavu kwa msingi kuwa wale tano wa kwanza ndio wanaoashiria
Kanisa ilhali wenzao wanaashiria walimwengu (watu wasio na imani katika Kristo
Yesu). Hebu tutazame vema maelezo tunayopewa kuwahusu.
Wote
kumi ni wanawali/mabikra
Wote
kumi walialikwa sherehe kumlaki bwana harusi
Wote
kumi walitwaa taa zao ila tano kati yao ndio walio twaa pamoja na mafuta
katika vyombo vyao
Tokana na maelezo haya tunaona kuwa
wote walikuwa watakatifu bila unajisi wo wote; ubikra,(2KOR. 11:2). Tena wote
walikuwa wamealikwa katika sharehe ile kumlaki bwana harusi, hii ina maana kuwa
walikuwa na ufahamu wa harusi ile na zaidi walikuwa maswahibu ama ukipenda
wandani wake bwana harusi kwa lile jukumu waliloteuliwa kutimiza, yaani,
kumlaki atakapowasili. Isitoshe wote walitwaa taa zao, kuonyesha walikusudia kuwa
bwana harusi angelichelewa kwa kuwa hakuna aliyetamauka na kwenda, bali
walimngoja hadi usiku wa manane, hii ina ashiria imani yao. Sawa na hayo, taa
kama tujuavyo huashiria Neno Takatifu la Mungu, (ZAB.119:105) na mafuta huashiria
Roho Mtakatifu, (KUT. 29:7; 1SAM. 16:13). Kama wote ni watakatifu na wateule
zake bwana tena wenye imani kwake na wanalishika neno lake (taa), basi mbona baadhi
yao (wale tano wapumbavu) hawakuruhusiwa kuingia harusini licha ya bidii yao na
kujitolea kwao?
Wapendwa kama tulivyoona wote kumi
walikuwa hali sawa isipokuwa kwa mafuta. Kama nikujitenga na ulimwengu na yote
yanayoweza tia utakatifu wao najisi wote walifaulu. Kama ni kuwa na imani kuwa bwana
harusi atakuja wote waliamini. Tushikilie hapo kwanza, na kutazama kuwa wote ilifika pahali wakasinzia na kulala, maanake
ni, imani ya kuwa bwana harusi atakuja ili didimia sawa na kukawia kwake
kulivyo zidi; kukawia kule kunaashiria majaribu. Ila bwana harusi alipowasil na
wote wakatoka nje kwenda kumlaki kuna wale kati yao hawakutwaa mafuta pamoja na
taa zao kwa hiyo taa zao hazikuwaka. Kuzimika kwa taa zile kwa kukosa mafuta
kunaashiria kupoteza imani na Neno la Mungu na badala yake kutegemea matendo makavu pekee. Vile vile, kutokuwa na mafuta kunaashiria kutopokea ubatizo wa Roho
Mtakatifu. Na huku kukosa mafuta ndio sababu ya taa zao kuzima na kutoweza kuwaka
tena, hali kadhalika ikiwa ndiyo sababu yao kufungiwa nje na kutokubaliwa
kuingia katika sherehe pamoja na bwana harusi. Kumbuka ilimfaa kila mmoja awe
na mafuta chomboni mwake. Naye bwana harusi siye mwingine ila ni BWANA YESU
KRISTO, (YN. 3:26-29).
Naye ndiye anayetueleza kupitia
mfano huu kuhusu kuja kwake, ili tujiweke tayari kwa kutimiza yote yanayohusu
imani na utakatifu. Na tunapofanya hivi isiwe kwa akili zetu tu na vile
tunavyodhania mambo yatatukia, bali tumtegemee Roho Mtakatifu kutuangazia Neno
lake hadi mwisho ili taa la tumaini letu lisizimike kwa kukosa mafuta wakati
giza na majaribu yatakapozidi na Bwana wetu aonekane kukawia kuja, (YN.
16:13-15). Fika hapa, tunaona wazi kuna baadhi ya Wakristo watakaoachwa nyuma
na Bwana atakapowakujia waliowake, (MAT. 7:21). Bali wapendwa isiwe hivyo kwetu
sisi, nafasi baado tunayo hivi sasa kubadili mienendo yetu na hususan mtazamo
wetu kuhusu Neno Takatifu; tuitisheni Roho Mtakatifu, na kutegemea uweza wake
ili atuimarishe katika imani kwa kutuongoza katika kweli yote na kutupasha
mambo yatakayotendeka hadi atapokuja BWANA YESU KRISTO kutuchukua. Na atakapokuja sisi tutamlaki
kwa furaha, shangwe na nderemo maana atatupata tukiwa watimilifu kumpokea na bila shaka atatukubalia
kuingia pamoja naye mbinguni alikotuandalia sherehe, (UFU. 19:9).
Sijazungumzia
wanaouza mafuta, hawa ni makuhani/watumishi wa Mungu (ISA. 24:1-3; MAT.
7:21-23)
No comments:
Post a Comment