NYAKATI NDIZO HIZI
Neema
na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
Watakatifu katika Yesu
Kristo, uyo huyo aliye utimilifu wa Mungu, natumshukuru kwa wema na rehema zake
ambazo Yeye huzifanya upya kila uchao. Kuhani Mkuu na Mkombozi wetu, unayetulingania
mbele za Mungu Baba pasi na kuchoka, tujalie uweza na neema zako. kwazo tukaweze enenda
katika njia zako hatua kwa hatua, siku kwa siku, tukikutazamia kufunuliwa
kwako. Ewe, shauku ya nyoyo zetu, Mtakatifu wa watakatifu, twakuomba msamaha
kwa maovu tunayokutenda; katika usemi, kutenda na hata dhana zilizoko ndani yetu. Maana, mbele
zako giza ni kama weupe wa mchana, hakika hakuna kinachofichika machoni mwako,
yote wayaona yote wayajua. Ewe, mwingi wa fadhila tuonee huruma na ututangulie
katika kila jitihada na juhudi, kutuweka mbali na maovu twakuomba na zaidi utuvute
karibu nawe. Muumba na Mwokozi wetu, twajisalimisha kwako utumiliki sisi
uliokomboa kwa kifo cha Mwanao, na kwa kufufuka kwake ukatupea uweza
wakufanyika wana wa Mungu. Ahsante, kwa Biblia Takatifu, nuru ituangaziayo njia
na kwa Roho atuwezeshae kuenenda kama, Ewe, Kristo. Amin.
Wateule kwa neema ya
Kristo Yesu, natumai baado twazidi kukaza mwendo huku tukisali na kusoma Neno
Takatifu, ili kuzilinda nafsi zetu tusije tukachukuliwa na dhihaka wala na
tamaa za zamani hizi tuishio, (2PET. 3:3-4). Wapendwa wa Mungu, tufurahieni kwa
ajili ukombozi wetu ukaribu, (RUM.
13:11-14). Nitawahimiza tena, tuzidisheni uaminifu na utakatifu katika mambo
yote tukikumbuka kuwa Mungu hakawii kutimiza ahadi zake bali huvumilia ili
apate kuwaokoa wote, (2PET. 3:8-18). Bw. Yesu, alipoulizwa kuhusu nyakati za
mwisho alizifananisha na zile za Nabii Nuhu. Zamani zile Nuhu alipopata maono
ya gharika itakayo angamiza dunia,wanadamu walijishughulisha na anasa za mwili
pasi na kutambua makusudio ya Mola wao. Ingawaje Nuhu alilihubiri lile Neno; wenye
kucheka na kudhihaki hawakukosa, hasa ikizingatiwa dunia ile haikuwahi shuhudia
mvua wacha mafuriko. Lakini kwa imiani na kuliheshimu Neno la Mungu, Nuhu
akapuuza hayo yote nakutimiza mashauri ya Mwenyezi, Muumba vyote, kwa kujenga
Safina, (MWA. 6:1-8; MAT. 24:36-41; 2PET. 3:5-7). Kama kawaida ya wanadamu,
walizidisha matusi na kumuudhi hadi alipoingia ndani ya Safina pamoja na aila
yake na mvua ikaanza kunyesha. Kwa hiyo Mkristo mwenzangu usishangae utakapo pokelewa
sawa na Nabii Nuhu huku ukibidiishwa na Roho kubadili nia na mwenendo wa maisha
yako ukitazamia kuja kwake Kristo.
Kadhalika, tuliona
jinsi Mwenyezi atakavyo ifariji dunia na kuifanya upya, katika Siku ya Sita; Kipindi
cha Faraja. Siku hii Mungu atawafuta wanadamu machozi yao na pia atawasamehe wana wa Israeli
kwa uasi wao. Lakini kabla ya hayo, fahari yote ya wanadamu, kiburi chao na utukufu wao utashushwa
hadi chini kabisa, (ISA. 2). Mwenyezi atatukuzwa na Yeye pekee ndiye
ataheshimika na kuabudiwa na wote waishio duniani. Sadfa na hayo, mpangilio aliouweka
Mwenyezi kwa viumbe wake utarejea; watoto watawaheshimu wazazi wao, nao vijana
watawaheshimu wazee, na mke atamheshimu mume wake, na mume atampenda mkewe.
Kipindi
hiki ndicho Nabii Isaya aliona katika maono na kuhubiri akisema mwanamume mmoja
atashikwa na wanawake saba wakiomba awaowe, (ISA. 3:13-4:6). Hapa ningependa
uone jinsi mwanamume atakavyo adimika kiasi cha kutukuzwa machoni pa wanawake saba:
Yeremia aliiona siku hii nakutabiri akisema, “Bwana ameumba jambo jipya
duniani; mwanamke atamlinda mwanamume,” (YER. 31). Hakika Mwenyezi atarejesha
kwa utimilifu mpangilio wake katika dunia yote. Pia nigependa urudi hapo kwa unabii wa Isaiya na uone jinsi
Mungu anatilia manani mapambo katika maovu atayohukumu. Mapigo haya kamwe
hayafai kukupata wewe binti wa Kristo, maana, wewe uzao wako na desturi yako ni tofauti,
sawa na urembo na mapambo yako, (1PET. 3:3-6). Vile vile katika kipindi hiki cha Sita, Mungu atawasamehe na kuwastarehesha watu wake wana wa Israeli chini ya utukufu wake.
Mabaki ya Israeli sawa na mabaki ya mataifa watamkumbuka Mungu na kumhimidi
yeye pekee (ISA.12:1-6; SEF. 3:8-20). Isitoshe, mamlaka na uongozi atapewa mfalme
atakayetukuzwa na Mungu duniani kote, (ZAB. 72).
Fauka ya hayo, tuliona kipindi
cha mwisho: Siku ya Saba, na jinsi kitakavyo kuwa kifupi. Kipindi hiki ndicho
kilichotabiriwa kuwa cha dhiki kuu ulimwenguni kote. Dunia itasononeka, sababu ikiwa hii ndiyo enzi ya Mpinga Kristo aitwae Asi, (Dan. 7:15-28). Bw. Yesu katika
kujibu wanafunzi wake kuhusu nyakati za mwisho alitabiri kipindi hiki, (MAT. 24:21-31). Hata katika chuo cha Ufunuo wa Yohana ambacho kimeshughulika na vipindi
vitatu vya mwisho pia kimefafanua mengi kuhusu enzi hii ya kumalizia historia ya
ulimwengu, (UFU.11-18). Cha msingi hapa nikuwa licha ya udhalimu utakaotekelezwa
na Asi dhidi ya Wakristo, Mungu Baba hatawaacha wanawe bila usaidizi. Mashahidi
wale wawili (Henoko na Elijah), watakuwa kikwazo kikuu kwa kazi zake, yule mwovu
na zaidi watawatia waumini ukakamavu na kwa ishara na miujiza za kutisha
watathibitisha uweza na mamlaka ya Mungu juu ya wote.
Baada ya mambo hayo yote,
mbingu zitafunguka na MFALME WA WAFALME atakuja kufanya vita na ulimwengu;
atawapiga kwa upanga wa kinywa chake na kuwachunga kwa fimbo ya chuma. Miaka ya
ufalme wake BWANA WA MBWANA itakuwa elfu moja (1,000), na Shetani pamoja na mapepo watatiwa
mbaroni chini kuzimu kwa muda huo wote. Ufufuo wa kwanza utafanyika wakati huu,
na wote waliouawa na Asi kwa ajili ya ushuhuda wa Bw. Yesu watafufuliwa; heri na
mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya
pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala
pamoja naye hiyo miaka elfu.
Miaka elfu itakapokwisha,
Shetani ataachiliwa na kuelekea kuwadanganya na kuwakusanya mataifa kufanya
vita na Bw. Yesu Kristo na wateule zake. Pindi tu, watakapozunguka Yerusalemu
moto utashuka toka mbinguni na kuwamaliza wote. Kisha BWANA atashusha kiti
chake cha enzi, mbingu na dunia zitakimbia mbele za uso wake na wote tangu
Adamu watafufuliwa, siku hii ndiyo Siku ya Kiyama, na hukumu itafanywa. Ole,
kwa wote watakao fufuliwa katika ufufuo huu wa pili na majina yao yakosekane
katika kitabu cha uzima. Hawa watahukumiwa mauti ya pili na kutupwa katika lile
ziwa la moto wa milele na milele. BWANA atapotimiza hukumu, atazifanya mbingu
na dunia mpya, Yerusalemu takatifu mji wa Mungu aliowatayarishia waaminifu ao
hao wateule zake itashushwa na Mungu Baba atafanya maskani yake pamoja na
wanadamu. Atakaa pamoja na wanadamu na atawafuta kila chozi toka machoni yao,
wala mauti haitakuwapo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu
hayatakuwepo tena. Maana, yote ya kwanza yataisha na Mungu atayafanya yote kuwa
mapya, (UFU. 19-22).
Natumhimidi Yeye aliye juu, na kumsifu na kumheshimu
Yeye aishiye milele; kwa maana enzi na mamlaka Yake ni ya milele hadi milele na
matendo Yake yote ni kweli, na njia Zake ni za adili. Na atukuzwe Bw. Yesu Kristo, Utimilifu wake Mungu wa Kweli
mbinguni na ulimwenguni kote. Hukumu na Mamlaka yametiwa mikononi mwake; ndiye
MFALME WA WAFALME NA BWANA WA MABWANA. Amin.
No comments:
Post a Comment