TUNU YA MOYO WANGU
TUNU
YA MOYO WANGU
Nitanena
bila sitara pasi na kuficha, utengano kuufisha upatano ututhibitikie,
Naam,
mawazo ya moyo wangu sitakuficha, siri ya mtima wangu nikufunulie,
Laazizi hakika
kama we'e sina hata pacha, mboni la jicho langu sogea unigeukie,
Ewe
tunu ya moyo wangu sogea, tusemezane kipenzi changu.
Kibri
na purukushani hazitokufaidi, sichukulie nitashtiti mwenyewe tasadikia,
Takufukizia shauri langu kama udi, ingawa shubiri nafsini tapenya shalikia,
Ungelirekebisha
kamwe singekuridi, na katu sitochoka mema kukutakia,
Ewe
tunu ya moyo wangu rekebisha, ufaidike kipenzi changu.
Uhodari
wako nautambua sawa na udhaifu wako, si mie kakufanya jinsi ulivyo,
Kwa
udongo nikaifanya misingi yako, kindakindaki nakufahamu kwa hivyo,
Ila tafakari
fahari yote ya maisha yako, yote hudumu kama umande ukaavyo,
Ewe
tunu ya moyo wangu tafakari, bila mimi huwezi kipenzi changu.
Tangia
mwanzo nilikujuza mapenzi yangu, nilikufanya uwe wangu wakipekee,
Ulimwengu
nalikupa ishara la penzi langu, na vyote nikavitiisha uvimiliki wee,
Roho
nikakujaza ushiriki utukufu wangu, chema nilichokuzuia nikipi niambee,
Ewe
tunu ya moyo wangu niambee, nijuze nikijue kipenzi changu.
Japo
maliki nilikuumba ukafanywa mtumwa, dhawabu na mamlaka ukayapoteza,
Kakutahadhirisha kwa Neno, ishara, na miujizwa, ila karidhia hila za Mnyang’anyi kikutongoza,
Hukunisadiki hata nilipokuamba atakuuwa, kongwa akakuvisha yakakupata niliokukataza,
Ewe
tunu ya moyo wangu nisadiki, nikukomboe kipenzi changu.
Nikasubiri
tena kwa saburi sikuoni, mchana kutwa sikuoni usiku kucha uwapi?
Dhalim kakuziba masikio kakupofusha machoni, kakulemaza usinirudie Ewe wangu waridi!
Haki kadai fidia ajili ya wako uhayawani, arbuni kiasi cha bikra kalipa tena kwa
hiari,
Ewe
tunu ya moyo wangu uwapi, nakudhamini kipenzi changu.
Uhai pia nikatozwa kutosheleza fidia, Utimilifu wa Mungu kautwikisha utumwa!
Aibu,
mateso, dhambi hata mauti zote kalipia, dhawabu yako na mamlaka kazitwaa,
Sasa
Mimi Ndimi Njia, Kweli, na Uzima, nifuate, nisikize na unitumainie daima,
Ewe
tunu ya moyo wangu nifuate, twende zetu nyumbani kipenzi changu.
No comments:
Post a Comment