Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
Watakatifu katika Kristo Yesu, ilmuradi muda u-pamoja nasi tuzidi kumtukuza na kumhimidi Mungu Baba wa mbinguni ambaye kwa neema ya kipekee ametufanya tuwe manukato yanayopendeza hapa duniani, juu mbinguni na ulimwenguni kote. Kwa kudura zake ameturehemu na kwa neema iyo hiyo katika Kristo Yesu akatupa uweza kuwa wana wa Mungu aliye hai kwa asili ya Roho. Ili daima tuenende kwa nia ya Roho wa Kweli ambayo ni uzima na amani, tofauti na nia ya mwili ambayo ni dhambi na hatima yake mauti; utengano wa milele na Mungu Baba. Kwa hiyo, Ewe Mungu Baba, shauku ya nyoyo zetu tunakutukuza na kukuhimidi kwa makuu ambayo umetutendea, huku tukikuomba uzidi kututawala na kutuongoza milele. Amin.
Wapendwa zake Mwenyezi, natumai twazidi jibidisha ili tuwe tayari kwenda naye atakapotujia, kama tulivyoona wiki jana kwa mwongozo wa Neno Takatifu. Nasisitiza, ahadi ya kuja kwa Bwana Kristo Yesu; kama mwizi bila kukusudiwa, i-pamoja nasi katika kizazi hiki. Walakini, najua wengi hapa watayazungusha macho yao na kukinai, wakisema, tumeambiwa mpaka tumechoka. Watu wengi wamejitokeza na hata wengine kati yao wakiapa kwa uhakika wakitaja tarehe na wasaa wa kurejea kwake Mwokozi kwa utukufu, bali yote yakaishia kuwa upuzi mtupu. Sipingi hayo au kuyakataa. Hakuna aliye mgeni wa habari hizo ambazo sote twazifahamu nakushuhudia kuwa ni tungo za uongo zilizojaa hila. Ila, nawakumbusheni enyi wateule zake Kristo Yesu, yakuwa Maandiko yako wazi kwetu sote. Kadhalika, Roho wa Kweli aliye arbuni tuliyopewa na Mungu Baba, ambaye daima Yu shahidi wa kuaminika na aliye ndani yetu, kawaida Yake atatuongoza na atatufunza yote ya kweli ili tuwe watimilifu katika imani. Basi, tusitumainie mambo yakuambiwa tu, bali tuweni wenye hekima katika mambo ya Mungu Babaetu, kwa dua na kusoma Biblia Takatifu tukaweze kuthibitisha au kubatilisha jambo lo lote. (1YOH. 4:1; 1KOR. 2:5-13; RUM. 8:9).
Licha ya hayo, wiki jana tuliifikia Siku ya Tano. Siku ambayo tulitambua wazi wazi kuwa ni hii yaendelea na kwamba sisi tulio hai hivi sasa twaishiriki siku kwa siku. Sawa na hayo, tuliona jinsi siku hii inafananishwa na kipindi cha Madhila. Sababu kuu ikiwa hukumu ambazo Mungu Mwenyezi, atatekeleza katika kipindi hiki ili kuutakasa ulimwengu mzima dhambi za wanadamu. Kioo cha enzi hii twakipata katika Agano La Kale; katika enzi ya ufalme wa Manasse hadi pale Yuda ilipotekwa na Mfalme Nebukadneza, (2FAL. 21-25). Falme hizi isipokuwa Ufalme wa Yosia, bila shaka zilisheheni ujeuri, dhambi na machukizo yakilaaina. Wana wa Israeli huku wakiongozwa na wakuu wao, walimtusi na kumchokoza Mungu Mwenyezi, kwa kuasi imani ya kweli na kudharau wema na rehema zake Jalali.
Walivuka mipaka kwa matendo yao na kunajisi ibada takatifu na dhabihu za Mungu wa Israeli, Muumba wa vyote. Sio tu, kwa ibada za sanamu walizoleta mpaka hekaluni na kuzijengea madhabahu; upumbavu wa Mfame Manasse kumtoa mwanawe mchanga kafara kwa miungu hii ya sanamu hapo hekaluni; Kuijaza Yerusalemu na damu isiyo na hatia; kuwatesa, kuwafunga hata kuwauwa walio Makuhani na Manabii wa kweli; zaidi ya udhalimu huu wote waliwapotosha watu wasimhimidi wala kumwabudu Mungu wao! Je, Mkristo, matendo haya si sawa na yale tunayoshuhudia kila uchao? Wakuu wa mataifa wanafunza na kuhalalisha yale Mungu, katika Neno lake Takatifu ameyasema ni mwiko, dhambi na machukizo. Isitoshe, wanaleta ibada izo hizo Kanisani mbele za Mungu. Kama vile, kuwaapisha wachungaji wasenge na wasagaji, kuidhinisha ndoa za mabasha; watu kufunzwa kuwatoa watoto wao kafara kwa ajili ya maisha mamboleo (uavyaji mimba) na kudhamini baraka za mali zaidi ya Mungu mpaji wa yote. (ZAB. 127: 2-5; LAW. 18:21-26; MAT. 22:37-40)
Wakristo, kama ushahidi ni huo basi tusidangayike ati kizazi hiki kitaepuka hukumu zake Muumba, Hakimu wa ulimwengu wote. La hasha! Mwenyezi katu hapotoshi haki wala hamheshimu mtu ye yote awaye Yule. Maana, Kanisa sio kazi ya wanadamu ili waichezee wapendavyo wao, bali Kanisa ni Mwili wa Kristo. Msingi wake Mungu Baba kauweka kwa kifo cha mwanawe wa kipekee Yesu wa Nazareti pale msalabani. Hivyo basi, kuliguza Kanisa ni sawa na kumchoma Mwenyezi mboni la jicho. Ole, wetu wanadamu kwa kudunisha na kudharau upendo wake Karima, huku tukijihangaisha na yale yasiyo na umuhimu. Jamani! tumrudieni Mungu Baba, kwa toba ya kweli, ni mpole wa hasira na mwepesi wa kurehemu, atatutakasa na kutuondolea ghadhabu zake asitumalize. Lau sivyo, nani awezaye kuzima ghadhabu zake? Wapendwa, tusighairi kutafuta msamaha wake, ila tufanyeni upesi kuzikimbilia rehema zake tukapate kuokoa maisha yetu pamoja na nafsi zetu. Kinyume na hayo tutashuhudia ulimwengu wote ukizama katika usumbufu na majanga makubwa ajabu. Wapendwa, sitachoka kuwasihi kwa uwezo wa Kristo Yesu, tufanyeni toba ili tujiepushe na hasira ya BWANA WA MAJESHI. (KUT. 34: 5-7; ISA. 1:18-20; JER. 30:5-11; UFU. 6:12-17).
Mwenyezi na atuhurumie. Turekebisheni njia zetu, maana, masumbuko ya Yakobo yako pamoja nasi, (UFU. 6:12-17; 8:1-13; 9:1-21). Msimu huu, utazidi kushika kasi na nguvu kwa ajili ya wingi wa dhambi zetu, na katika kutimiza haki Mungu Baba, ataihukumu na kuitakasa dunia kwa mapigo makuu. Haki itakapo timiza mahitaji yake, kipindi cha madhila kitapita na wachache watakaosalia duniani watalaki kipindi kipya cha Faraja, yaani, Siku ya Sita itaanza, (UFU. 10:1-6). Kipindi hiki kipya sawa na zama za Edeni, kitakuwa kifupi. Wanadamu, sawa na wazazi wetu; Adamu na Hawa, hawatadumu katika uwepo wa Mungu Baba. Mara tu, wataasi na kuichafua dunia kwa kila aina ya maovu. Watakapoasi, Siku ya Saba au kipindi cha Dhiki kitaingia, (UFU. 11-13). kinpindi hiki kitakuwa kifupi mno, kitakuwa si zaidi ya miaka Saba. kufupishwa huku ni ithibati ya huruma zake Karima, kwetu sisi waja, maana tuviumbe dhaifu na zaidi kwa ajili ya wateule zake, (MAT. 24:21-31). Yafuata ni mukhtasari wa siku hizi mbili za mwisho, yaani, Siku ya Sita na Siku ya Saba mtawalia.
SIKU YA SITA
(MWA. 1:24-31)
|
HISTORIA YA ULIMWENGU
|
KANISA LA FILADELFIA
(UFU. 3:7-13)
|
Siku hii inafananishwa na kipindi cha Faraja.
Mungu ataufariji ulimwengu tokana na mateso yake yote na kuijaza
dunia yote amani, furaha na upendo. Sadfa na hayo watu watamjua Mungu Baba, watamwabudu
na kumhimidi kwa kweli.
Lakini sawa na siku hii ambapo wanyama wa nchi kavu waliumbwa
pamoja na mwanadamu, baado tamaa za mwili na nia yakujitawala nafsi zao
wenyewe itakuwepo pamoja wanadamu.
|
Katika Agano la Kale kipindi
hiki kilianza na utawala wa Koreshi Mfalme wa Uajemi (Ezra, 1:1-3). Zama hizi
zilishuhudia mabaki ya Israeli na waliorudi toka uhamisho wakimrudia Mungu
wao wakimhimidi na kumwabudu Yeye pekee. Kuwekwa kwa msingi wa Hekalu jipya
na kujengwa tena kwa kuta za Yerusalemu.
Tofauti na kipindi cha
madhila ambacho kitatamatika kwa kilio na majonzi makuu. Katika kipindi hiki Mungu
atawafuta machozi wanadamu wote. Kutakuwa na utulivu, kuondokewa na shida
pamoja na masaibu yote yaliyoukabili ulimwengu. Upendo wa Mungu utashuka
duniani na wanadamu watapendana na watamwabudu Mungu wa kweli katika Kristo
Yesu.
|
Kanisa la zama hizi, litapewa mlango uliofunguliwa
mbele yao wala hakuna awezaye kuufunga.
Wale watakaolishika Neno la Bwana watakuwa
wachache hapo mwanzo na wenye nguvu kidigo
Wayahudi watatubu na kumtambua Kristo Yesu na
kumwabudu
Waumini watalindwa na saa ya uharibifu
itakayoijilia ulimwengu wote
kuwajaribu wakaao juu ya nchi.
Zaidi, Bwana anasisitiza kuwa yuaja upesi.
Kwa hiyo wanahimizwa kushika sana walicho nacho (imani ya kweli) ili wa
hifadhi taji zao.
Washindao kwa kutoachilia imani watafanywa
nguzo katika hekalu la Mungu na hawatatoka huko tena.
Vile
vile, Bwana ataandika jina la Mungu Baba na jina la mji wa Mungu; Yerusalemu
mpya ishukao toka mbinguni kwa Mungu juu yao.
Isitoshe Kristo Yesu aliyetukuzwa
ataliandika jina lake jipya juu yao. (Baraka na neema ziliyoje).
|
SIKU YA SABA
(MWA. 2:1-3)
|
HISTORIA YA ULIMWENGU
|
KANISA LA LAODIKIA
(UFU. 3:14-22)
|
Siku hii inafananishwa na kipindi cha Dhiki.
Sawa na siku ya Saba aliyopumuzika Muumba baada ya kumaliza
kazi zake zote alizozifanya. Vile vile katika kipindi hiki Mungu atapumuzika tokana na kazi zake!
|
Kipindi hiki ndicho mwanya
uliopo kati ya Agano la Kale na Agano Jipya. Ulikuwa ni mwanya wa miaka 400
ya kuadimika kwa Neno la Mungu. Kipindi hiki kiliendelea hadi kuja kwake Yohana Mbatizaji.
Kipindi hiki kimetengewa
wote walio kataa Kweli. Kadhalika, kipindi hiki ndicho kitakacho shuhudia ule
aliyetabiriwa na kuitwa Mpinga Kristo au Asi.
Atazaliwa kwa kutenda kwake Shetani na
atakuwa na uwezo wa ajabu na kutenda ishara za uongo, (2THE.2:8-12). Atakuwa
dhalimu kupindukia na atawatesa wanadamu kwa mateso ya ajabu na kutisha ususan
Watakaomgeukia Kristo Yesu kwa imani.
Inatupasa tumshukuru Mungu Baba daima kwa
uaminifu wake na upendo wake wa ajaabu na usiobadilika. Maana katika dhiki
hii, Mwingi wa huruma, Babaetu wa milele hatoridhia kuwaacha wanadamu bila
usaidizi. Atawarejesha Henoko na Elija duniani waweshahidi zake, na kwa uweza
mkuu ishara na miujiza watahubiri Kristo Yesu Mwokozi wa ulimwengu wote.
|
Tofauti na Makanisa hayo mengine Bwana
anaanza kwa kulisuta Kanisa la zama hizi; matendo yao si baridi wala si moto.
Kwa ajili ya uvuguvugu wao Bwana anawatapika
toka kinywa chake.
Kiini cha uvuguvugu wao ni utajiri wao mali.
Bali Bwana awatambua kuwa wanyonge, wenye mashaka, masikini, kipofu na walio
uchi.
Ni kwa upendo ana wasuta na kuwakemea vile
ili waje kwake, awatibu upofu wao, awavishe nguo na kuwapa dhahabu ya kweli.
Anawajulisha Yu mlangoni anabisha na yeyote
atakayemfungulia watakula pamoja.
Na yeye ashindaye ataketi pamoja na Bw. Yesu
katika kiti chake cha enzi sawa na Kristo Yesu alivyoketi pamoja na Mungu
Baba baada kushinda majaribu na mateso yake yote.
(Mungu Baba kweli ni wa maajabu. Rehema na Baraka zake ni za
milele hata milele). Amin.
|
No comments:
Post a Comment