Tuesday, 12 August 2014

VIPINDI SABA VYA NENO LA MUNGU (SURA 2)



Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.



Enyi aila yake Mungu wa kweli, Muumba wa mbingu, dunia, ulimwengu na vyote vilivyomo, natuishikeni itikadi yetu ya Ukristo kwa kumtukuza Mungu kwanza:- Daima mwaminifu na daima mkweli, ndani yake hamna hila wala hata chembe cha uovu hakiwezi patikana karibu ya uvuli wake, kwa kuwa Ewe, ni nuru na mwanga wala hamna hata giza katika uvuli wake. Ndiye aangazaye njia na kutuelekeza sote kwa mapito yaliyonyooka ambayo huishia uzima wa milele. Amin.



Wapendwa, kwa neema yake Mungu Baba katika Kristo Yesu, leo hii tutaendeleza mada tuliyoianza wiki jana ya kujifahamisha nyakati na misimu. Natumai sote twafahamu umuhimu wa kujua na kuelewa vema nyakati, hususan msimu tunaoishi ili tusipatikane kama wanawali walioishiwa na mafuta wakati bwana harusi alipochelewa kuja au kama mtumwa aliyetelekeza majukumu yake, (MT. 25:1-13; LK. 12:42-46). Siku zote wateule wa Mungu, yatupasa kuwa tayari kumpokea Bwana wetu maana yeye mwenyewe atuonya kuwa yuaja kama mwizi wakati hakuna mtu anamkusudia, (LK. 12:35-40). Basi tuweni waangalifu kwa kukesha tukiomba na kulisoma Neno Lake daima ili tupatikane tayari na wastahiki wa kuingia karamuni naye tamanio la moyo wetu, Bw. Yesu Kristo.



Wiki jana, tuliangazia vipindi vitatu vya kwanza na hapa ndipo tutachukulia na kuangazia vipindi viwili kama inavyofuata;

 

SIKU YA NNE
(MWA. 1:14-19)
HISTORIA YA ULIMWENGU
KANISA LA THIATIRA
 (UFU. 2:18-29)

Siku hii inafananishwa na kipindi cha Uangazo.



Kipindi hiki kilishuhudia umoja na ushirikiano wa kanisa ukigawanyika kuwa madhehebu mawili; Ukatoliki na Uprotestanti. Isitoshe, mamlaka na elimu zikatofautishwa baina yale ya dini na ya ulimwengu. Migawanyiko hii kupitia madhehebu yake madogo madogo pamoja na mashule na vyuo vya kila aina, ikaeneza nuru kote duniani. Wanadamu wakila-tabaka na kila nchi duniani wakafikiwa na dini pamoja na elimu.

Sawa na mianga ile miwili ambayo Mungu aliifanya pamoja na nyota, vyote vitie nuru juu ya nchi na kutenga nuru na giza.

Katika Agano la Kale kipindi hiki utambulika kuwa kile ambacho kilifuatia kuaga kwa Mfalme Suleimani ambapo Taifa la Israeli liligawanyika mara mbili, kukawa na Israeli upande wa Kaskazini na Yuda upande wa kusini. Wakati huu, Mungu akawainuilia manabii waangaze nuru ya neno lake kwa watu wake ili kuwatenganisha na giza ya maovu waliotenda sawa na mataifa mengine.



Kipindi hiki kilianza na mgawanyiko wa umoja wa Kanisa uitwao “Reformation” na kuendelea wakati wa “Industrial Revolution” hadi kumilikiwa kwa mataifa madogo na yale yenye uwezo (ukoloni).



Kanisa la msimu huu lilitambulika kwa matendo, imani, huduma na subira. Maana katika kipindi hiki ndipo watu wengi walijitolea maisha ya utawa na umishonari kuenenda wasipokujua kulihubiri Injili. Wegine wakijitolea kwa huduma mbali-mbali kwa hali na mali aidha kufadhili, kuasisi na kundikwa kazi hata kujiunga pasi na kutarajia malipo yo yote.

-Lilitambulika kwa matendo, imani, huduma na subira.

-Mgawanyiko kwa mafunzo ya Yezebeli Nabii wa uwongo aliyefunza, kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu na uzinzi

-Bwana naye awaapia hukumu wale wakosaji na urithi wa mamlaka ya kutawala mataifa kwa fimbo ya chuma kwa wale waaminifu.
 

 

SIKU YA TANO
(MWA. 1:20-23)
HISTORIA YA ULIMWENGU
KANISA LA SARDI
(UFU. 3:1-6).

Siku hii inafananishwa na kipindi cha Madhila.

Kipindi hiki kimejaa ubishani, fujo na mashindano. Kila mtu  akitaka kuitawala nafsi yake mwenyewe. Desturi za Ukristo hazi  heshimiki wala kutambuliwa, uasi Mungu umekidhiri mpaka ndani ya Kanisa. Wanadamu wanajishugulisha na haja zao za mwili peke yake kwa hivyo dhambi imezidi  hata kupita mipaka. Kwa Kanisa, madhila makuu ya ungojea mwili wa Kristo, maana, dhambi inatawala kote hata Kanisani jambo ambalo Mwenyezi atarekebisha mwenyewe na kuutakasa Mwili wa Kristo na ulimwengu kwa hukumu za kutisha. 

Sawa na wanyama  ambao Mungu aliwafanya katika siku hii, kila mmoja huitawala nafsi yake na kuongozwa na tamaa zake. Ndivyo ulimwengu ulivyo katika enzi hii.

Katika Agano la Kale kipindi hiki kilianza na utawala wa Mfalme Manase. Utawala kuwa umejaa kila aina ya maovu na madhila kiasi cha kumkasirisha Mungu. Kinpindi hiki kiliendelea hadi pale wana wa Israeli walipoharibiwa na adui zao na kubebwa mateka hadi Babloni.



Kipindi hiki kilianza na vita vya Kwanza vya Dunia. Ambavyo vilichangia pakubwa kutanguka kwa ukoloni, mataifa walipopigania uhuru wa kujitawala wao wenyewe. Kipindi hiki ndicho tulipo  na baado cha endelea. Twajionea wazi wazi jinsi mambo yanavyoenda, maovu kutukuzwa na wema kudhalilishwa. Neno la Mungu linadharauliwa na kudunishwa peupe. Ulimwengu nao  unakazania kuhalalisha maovu na kuilazimu Kanisa kuhalalisha dhambi. Zaidi, watu wote hata watoto wanatambua na kuzipigania haki zao ili wazimiliki nafsi zao wenyewe.

Hapa Kanisa limeadhirika pakubwa kwa dhambi na kuwafanya wachungaji pamoja na viongozi wake wasiheshimike. Wale wanaofuata desturi na itikadi za Kikristo wanachukuliwa kuwa wajinga na washamba kupidukia, huku Kanisa likijibidiisha kufanana na ulimwengu kwa hali na mali.



-Kanisa lina jina la kuwa hai lakini limekufa.

-Matendo yake yamekaguliwa na kupatikana si-timilifu mbele za Mungu.

-Bw. Yesu analihimiza kutubu na kuimarisha mambo yaliyosalia kabla yaangamie.

-Hata hivyo kuna wachache kati yao ambao hawajatia mavazi yao uchafu.

-Zaidi ya hayo wanapewa onyo, wakeshe kwa kuwa Bwana atakuja kama mwizi bila hao kukusudia!

-Aliyemsafi atakwenda pamoja na Bw. Yesu na jina lake halitafutwa toka kitabu cha uzima na Bwana atalikiri jina lake mbele za Mungu Baba na malaika wake.

 

Inalazimu kutilia mkazo “Kipindi hiki cha Tano,” kisa na maana, ndicho kinachotuhusu sisi hivi sasa, ama, ukipenda ndicho twaishi na kushuhudia siku kwa siku. Kipindi hiki ni sawa na kile katika Agano La Kale, kilianza na Ufalme wa Manasse hadi kuanguka kwa Yerusalemu mikononi mwa Mfalme Nebukadneza aliyewatwaa wenyeji wa Yerusalemu mateka mpaka Babeli, (2FAL. 21-25). Unapo soma mambo yaliyotendeka chini ya wafalme wa Yuda katika kipindi hiki inastaajabisha jinsi matendo yale yanavyo fanana na yale yanayotendeka zama hizi! Isiokuwa Mfalme Yosia, wengine wote walijibidiisha kutenda kila uovu na kumkasirisha Mola pasi na kujali hukumu itakayo wafika sawa na neno lile Mungu alinena kwa vinywa vya manabii aliowatuma kati yao. 

 

Natuige waunimi wa wakati ule waliotakasika kwa kuzishika amri zake Mwenyezi na kuzitenda ndivyo nasi inatupasa kufanya wapendwa. Tusipotee kwa kuingilia anasa za ulimwengu huu wala kukubaliana na hila za zama hizi maana hukumu ipo karibu na wala Mungu Baba hatachelewa kulipa kisasi, dharau, matusi na chuki anazofanyiwa, licha ya kuupenda ulimwengu nakumtoa mwanawe wa kipekee ili kuukomboa. Tujitakaseni wakristo! Ahadi ya Bwana ipamoja nasi katika kizazi hiki sawa Kanisa la la msimu huu; Kanisa La Sardi. Kanisa ambalo Bw. Yesu alilihimiza kutubu na kuimarisha mambo yaliyosalia kabla hayaja-angamia. Zaidi ya hayo aliwapa onyo, wakeshe kwa kuwa atakuja kama mwizi bila hao kukusudia! Aliyemsafi atakwenda pamoja na Bw. Yesu na jina lake halitafutwa toka kitabu cha uzima na Bwana atalikiri jina lake mbele za Mungu Baba na malaika wake. Mkristo muda ushayoyoma na wakati ndio huu umewadia, je, utakwenda pamoja na Bwana atakapokujia wale waliosafi? 


 

No comments:

Post a Comment