Sunday, 3 August 2014

VIPINDI SABA VYA NENO LA MUNGU (SURA 1)

Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

 

Ndugu wapendwa, kama ilivyo desturi yetu Wakristo kabla ya yote ni kumtukuza Mola wetu mwingi wa neema kwetu sisi viumbe wake. Wema kwa wabaya hatelekezi kazi ya mikono yake kamwe, kwa kuwa Mungu Babaetu ni Jalali ambaye siku zote anatilia manani maisha ya kila mmoja ya waja wake. Makusudi, kutuongoza katika njia iliyonyooka, kutujulisha kweli na hatimae kuturidhisha uzima wa milele. Enyi aila yake Mungu wa kweli, tuzidi katika upendo wa Kristo Yesu; upendo usio na dosari yo yote, upendo ambao hututofautisha na jamii nyingine za ulimwengu na kututambulisha kuwa wana wa Mungu Muumba mbingu na dunia na vyote vilivyomo. 

 

Kadri ya ukarimu wake Babaetu wa mbinguni anatutunukuu kuona siku kwa siku tukiwa bukheri wa afya, ndivyo nasi ndugu zangu inatupasa kumtumainia na kuzitegemea kudura zake katika kila hali na kila njia. Yote haya kwa manufaa yetu wenyewe maana Mwenyezi hapungukiwi na chochote wala hakuna amfaidie kwa lolote, hata katika kutenda wema faida twajizulia wenyewe, (EBR. 6:10-12). Sadfa na hayo Wakristo wenzangu inatupasa kuzidisha bidii kusoma na kufahamu Neno lake huku tukikesha kwa sala na dua ili atuepushe na maovu ya ulimwengu huu. Kama tulivyo-tathmini wiki jana, uovu unatukuzwa hadharani na uhalifu dhidi ya Neno lake Takatifu kufanywa jambo la kawaida na kupigiwa shangwe hata na wakuu wa mataifa! Basi tutajiepushaje na upotovu huu ili nasi pia tusidanganyike na kujipata tukiwa tumesombwa na machafuko haya, (ZAB. 119:9-16). Nitasisitiza tena, Mungu ni Mtakatifu na hatawaacha wanadamu kumdhihaki na kumtusi jinsi wapendavyo wao huku wakisingizia maendeleo, sayansi, utajiri na maisha mamboleo, (MET. 14:11-12; 21:12). Linganisha hayo na yale mcha Mungu anajiwekea akiba kwa ulokole wake, (MET. 14:26-27). 

 

Kwa hiyo nivema kujijengea msingi imara, na Neno ndiye msingi huo. Kama tujuavyo vyote vilifanyika kwa Neno wala pasipo Neno halikufanyika lolote na ndani yake ndimo uzima na uzima huo ndio nuru ya watu wote, (YN.1:1-5). Nuru hii ndiyo iangazayo na kun’gaa katika giza wala giza haiwezi kuizidi katu. Sote twatambua hivi kuwa ni kweli, maana, ijapokuwa uovu umekidhiri Mola wetu hajatuacha bila nuru yake, hasha, kinyume na hayo anatueleza kinaganaga yakuwa Yeye ndiye Mungu atangazaye mwisho tangu mwanzo na shauri lake litasimama na mapenzi yake yote kutimia, (Isa. 46:10). Hivi nikusema kwamba yote yanayotendeka hayapaswi kututia jakamoyo, letu nikuishika imani kwa dhati maana yote haya aliyakusudia wala hakuna hata kimoja kinacho-endelea asichokijua. Kwa hiyo, tokea mwanzo Mungu Baba aliridhia kutufahamisha mpango wake kwetu sisi waja wake na katika Neno Lake Tukufu akatufichulia yote yatakayo tukia hadi mwisho wa dahari.


 



SIKU YA KWANZA
(MWA. 1:1-5)
HISTORIA YA ULIMWENGU
KANISA LA EFESO
 (UFU. 2:1-7)

Siku hii inafananishwa na kipindi cha Upanzi wa Mbengu.

Sawa na kuifanya Nuru katika Siku ya Kwanza; Mwenyezi akaanza mikakati ya kuijaza ulimwengu nuru (Neno Lake) ili kumkomboa
Mwanadamu aliyepotea katika giza.  


Katika Agano la Kale kipindi hiki hufahamika kama enzi ya kale; tokea kuanguka kwa Adamu hadi enzi ya Mababa wa Israeli. Kilitamatika Israeli wakiwa watumwa katika Misri.



Katika Agano Jipya kipindi hiki cha anza na kuzaliwa kwa Yesu Kristo hadi vifo vya Mitume Petro na Paulo.



Matendo ya Kanisa hili ni sambamba na yale ya Kanisa la kwanza, lililokuwa chini ya uongozi wa Mitume baada ya Bw. Yesu kupokelewa mbinguni.



-Adha na taabu kuu iliyowapata

-Kutochukuliana na watu wabaya

-Kuwajaribu mitume wauongo na kuwatambua

-Subira na uvumilivu bila kuchoka 

-Kuanguka na kusahau upendo wao wa kwanza (soma nyaraka za Mt.Paulo kupata maelezo zaidi).


 


SIKU YA PILI
(MWA. 1:6-8)
HISTORIA YA ULIMWENGU
KANISA LA SMIRNA
 (UFU. 2:8-11)

Siku hii inafananishwa na kipindi cha Utenganishwaji na Unyuyizaji.

Mwenyezi akaanza kujitengea watu wake duniani toka kwa mataifa huku akiwatendea ishara na miujiza za ajabu toka juu mbinguni. Sawa na alivyotenganisha maji  yale yaliyo juu kando na yale yaliyo chini.

Katika Agano la Kale kipindi hiki kilianza wakati Yusufu akiwa Misri. Mungu akaikomboa Israeli akimtumia Nabii Musa hadi siku za Nabii Samueli.



Katika Agano Jipya kipindi hiki cha anza amri ya Bw. Yesu kuwa wanafunzi wake wajitenge ili wabatizwe kwa Roho Mtakatifu, awape uwezo wakuihubiri Injili kwa mataifa yote. Tamati inakusudiwa ni mwanzo wa milki ya Konstantino.


Matendo ya Kanisa hili ni sambamba na yale ya Kanisa ilivyozidi kukua baada ya Mitume mpaka enzi ya Mababa wa Kanisa.



-Dhiki na umasikini wao kwa kuondokewa na Mitume walokwisha kuaga dunia.

-Utajiri wa imani licha ya kuhangaishwa na wayahudi (Sinagogi la shetani).

-Kutaabishwa kutupwa gerezani lakini mateso yakwisha karibuni

-Uhimizo wa kuwa waaminifu hata kufa na kwa hakika wataridhi taji ya uzima

-Yeye ashindaye hatapatikana na mauti ya pili.

 





SIKU YA TATU
(MWA. 1:9-13)
HISTORIA YA ULIMWENGU
KANISA LA PERGAMO
 (UFU. 2:12-17)

Siku hii inafananishwa na kipindi cha Amani.

Utulivu, kukua na kuongezeka kwa watu wa Mungu katika ulimwengu. Kukua kwa itikadi za kuabudu na desturi za kumcha Mungu kuujaza uso wa nchi. Sawa na maji kukusanywa pamoja ili ardhi itokezee na kufanywa kwa miche itoao mbengu na miti za matunda zizaazo matunda kwa jinsi yazo ili ziujaze uso wa nchi.



Katika Agano la Kale kipindi hiki hufahamika kama enzi ya Ufalme wa Israeli. Tokea Nabii Samueli, Mfalme Sauli, Mfalme Daudi mpaka Mfalme Sulemani.



Kipindi hiki cha anza na milki ya Konstantino haswa kuratibishwa kwa sheria ya amani iitwayo “Pax Romana” hadi uamusho uitwao “Renaissance.” Kipindi hiki kilishuhudia kuongezeka na kukua kwa Kanisa katika maeneo ya mataifa yote ya wakati ule.

Matendo ya Kanisa ya zama hizi yalishughulika kukuza imani na kuhifadhi itikadi na desturi za Mitume jinsi Kristo alivyowafunza. Ijapokuwa walikumbana na desturi tofauti za uabudu sanamu, mizimwi, uchawi, nakadhalika.

-Kushika sana jina la Kristo na Imani licha ya Shetani kuwa na kiti chake cha enzi kati yao.

-Hata hivyo baadhi yao walishika mafundisho ya Balaamu (kuvila vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu na kuzini)



No comments:

Post a Comment