Sunday, 27 July 2014

IMANI YA KWELI NI KUFAHAMU NA KUTENDA NENO LAKE (SURA 2)



Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

 


Ahimidiwe, Mungu Baba, juu mbinguni, hapa duniani na ulimwenguni kote. Kwa kudura zake ametuwezesha kupatana tena katika ukurasa huu, ili tukaweze kuzidi kuangazia yanayotukabili siku baada ya siku kwa minajili ya kufahamu nyakati tunazoishi. Tukidurusu kwa ufupi; wiki jana tuelekezea kurunzi kadhia ambazo zimekuwa zikiendelea hapa nchini na kuona jinsi Mwenyezi anavyotilia manani maisha yetu, na kutuepusha na uharibifu mara tulipoinua sauti zetu na kumlilia. Ahsante, zetu kwa fadhila zako Baba wa mbinguni. Walakini tusiache kufunga na kuomba hadi nchi yote itakapotulia tuli. Leo hii tutaendeleza mchakato wetu wa “imani ya kweli,” huku tukilenga kujinasua tokana na kasumba ya kutumainia mali.

 

Mwongozo wetu wa maisha kama desturi na itikadi ya Kikristo hutoka kwa Neno Tukufu la Muumba wa vyote:- Biblia Takatifu. Zaburi 49, sawa na chapisho la wiki ilopita ndio inatupa mwelekeo ufaao kwa mchakato huu. Wapendwa, sote twajua kuwa mali au utajiri una ushawishi mkuu tena wengi hushindwa kustahimili mshawasha wake kiasi cha kupoteza nafasi zao katika makao ya milele, MT. 19:16-24. Kunena hivi haimanishi tuchukulie aliyejari sawa na mtu aliyepotea, asilani! Utajiri ni Baraka toka kwake Karima anyegawia wote kwa hekima zake. Bali kufanya mali kuwa tegemeo na tumaini hapo ndipo mja hupotoka, LK. 12:13-21. Fika hapa najua wengi watasema mambo haya twajua vema. Nami nitawaulizeni kweli mwafahamu?

 

Kuuliza vile si kejeli bali nikutoa ilani ya mambo yanayotusibu! Wakristo hebu tujirudi wenyewe natuone jinsi Mwili wa Kristo (Kanisa) ulivyo adhirika kwa kuegemea mali, vilevile, serikali na asasi za utawala. Pakubwa mali na utajiri umefanywa chanzo cha kuheshimika na kukubalika katika jamii. Nao wenye mali wamekuwa ndio washauri wakutamanika na kuaminika, bora unacho utategewa sikio na kulimbikiziwa sifa sufufu. Fauka ya hayo utakwezwa na kufanywa kielelezo cha wengi licha ya utovu wa maadili na hata zaidi kukosa imani! Wahenga kamwe hawakukosea waliponena mavi ya tajiri hayanuki.a

 

Mambo haya kama tujuavyo yamechangia changamoto na taabu si haba katika Kanisa pamoja na utawala wa nchi; ushawishi mkubwa unaotukabili ukitokana na nchi tajiri duniani na zenye uwezo. Sio siri kuwa nchi hizi zimejizatiti kueneza na kufadhili upotovu na uovu wa kila aina duniani kote. Ole, wetu sisi wanyonge tutakapo acha mwongozo wa Biblia Takatifu na kushika mafunzo yao: Talaka; Usenge na Usagaji; Uafyaji Mimba; Uasi Mungu, ni baadhi ya uchafu unaopaliliwa duniani na hao matajiri wenye uwezo, na kubatizwa maisha ya kisasa. Bali wakristo tusichoke kuenenda katika uvumilivu na unyenyekevu mwishowe Mungu wetu atatufariji, MT. 5:1-13; LK. 6:20-26. Ijapokuwa  tutafinyika tunahakika kwa kinywa cha Kristo mwisho wetu ni mwema, tofauti na hawa wanaoupotosha ulimwengu, hao tusiwaogope wala kuzitamani njia zao, ZAB. 49:16-20.


 

Mbarikiwa ni ewe Mkristo unayejiwekea akiba mbinguni kwa matendo ya adili pamoja na kukesha na kuomba huku ukimtarajia Mkombozi, MT. 6:19-21; Lk. 19:11-27. Mwenyezi, aridhie kutunasua na uchu ya mali, bali atuzidishie uwezo na kaida ya kuenenda tukiwa imara katika hatua zetu tukifuata nyayo zake daima. Pamoja nakutenda haya tukumbukeni viongozi wetu wa Kanisa na Taifa, tuwapeane kwake Mchungaji Mwema ili awaongoze kule kwema kwa hekima na uweza. Zaidi tukumbukeni, hata katika taabu na majaribu ni vema zaidi kumhimidi Mungu kuliko mwanadamu, ZAB. 49:5-15.   

 



Natumhimidi Yeye aliye juu, na kumsifu na kumheshimu Yeye aishiye milele; kwa maana enzi na mamlaka Yake ni ya milele hadi milele na matendo Yake yote ni kweli, na njia Zake ni za adili. Na atukuzwe Bw. Yesu Kristo, Utimilifu wake Mungu wa Kweli ulimwenguni kote. Amin.

No comments:

Post a Comment