Sunday, 13 July 2014

IMANI YA KWELI NI KUFAHAMU NA KUTENDA NENO LAKE (SURA 1)



Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

   

Enyi wateule zake Haki, Ewe, Mwenye uweza wote, juu mbinguni, hapa duniani, chini kuzimu na ulimwenguni kote, kheri na fadhila zizidi kuwatangulia toka kwake Masihi wa Mungu uyo huyo aliye Ufufuo na uzima. Hususan katika kipindi hiki ambacho sote tunang’amua kuwa kimejaa changamoto tele nchini na dunia nzima. Tukichukulia hatua toka chapisho lililotangulia; Zaburi 40, nivema kutangulia kumshukuru Mungu, bila kuchelea kwa maana ametujalia neema zake ambazo ni za milele. Hebu tutafakari kwa kina yale yamekuwa yakitokea nchini; uvamizi, mauaji ya kiholela, milipuko na mashambulizi ya kigaidi, uhasama wa kisiasa na kwa ujumla utulivu kutupotea kwa kila hali! Kijumla twaweza sema, hali ya taharuki, majonzi na kiwewe ilikuwa imeigubiga mipaka yote ya taifa letu!

 

Licha ya giza kukaa kama ingetufunika, ghafla nuru ya amani ikachomoza! Swali la msingi litupasalo kujiuliza ususan sisi Wakristo ni:- nikipi hasa ambacho kilitendwa kwa mkono wa mwanadamu ili utulivu uanze kurejea? kama kawaida hapa wengi watatapatapa kwa visingizio vya kila aina na maelezo marefu yaliyosheheni misamiati utadhani ni mashindano yakutwikwa taji la kujieleza kwa ufasaha kwa Kimombo. Bali kando na sokomoko hizo zote aliye na macho hambiwi tazama, maanake, bila shaka ahsanta, zote nikwake Mwingi wa Rehema. Yeye, Rahmani mwingi wa Huruma ndiye katupandisha toka shimo la uharibifu na toka udongo wa utelezi. Enhe! Si kwa mkono wa yeyote ule ila kwa uweza wake Mungu wa Kweli. Yeye karidhia kutuepusha na uharibifu kwa kusikia kilio cha wanawe wateule; Wakristo. Bila kusitasita, itambulike bayana kuwa ni maombi ya Wakristo, kwa kufunga na kuombea taifa hili huku tukimlilia na kumgoja Mungu Baba kwa uvumilivu ndiyo yamefanya haya. (ZAB. 133; MAT. 18:18-20).

 

Wapendwa, tazameni makuu yanayotendeka Mwili wa Kristo; Kanisa, linapoamua kuenenda kwa umoja na kwa ujasiri wa imani! Kila wakati tunapochukua hatua sawa na Neno Lake Muumba mambo hutengenea sambamba na ahadi zake. Hivi ni kusema kwamba kama kweli tutamtegemea kwa kutimiza mapenzi yake maishani mwetu kila siku basi hatuna budi kuuona uweza wake mkuu ukitushindania kwa jambo lolote lile, (KUT. 6:6-7). Uhakika wa mambo ndio huo, na kama tunatambua hivi, basi nini hasa huwa kinatukwaza tusiendelee na moyo huo wa umoja na maombi? Na nilipi la busara kutenda ilitujiepushe na majanga kama haya kutufika tena? Majibu ya kuridhisha na ushauri nasaha hautopatikana kwengine ila  kwa Neno lake. Ni hapa tu, katika Biblia Takatifu pekee ndipo tiba ya magonjwa na matatizo yote yapo. Basi nakuulizeni kwa nini kujitaabisha kwa kuzurura huku na huko? Badala yake tujichoshe na kuvunjika nyoyo huku tukiwa wakavu, tukichekwa hata kudharauliwa na hao mahasidi wa imani yetu!

 

(ISA. 9:6). Sio bora zaidi tulivyotangulia kufululiza kusimama mwambani pahala ambapo hatua zetu ziliimarishwa kwa ajili ya dua. Hivi sasa nani hana wimbo midomoni akielezea utulivu ulorejea? Kama atupeavyo Jua na Mvua, wema kwa wabaya, vilevile amani hutufikishia sote. Wapendwa, nafanya kusisitiza ili tusikizane, maombi ndio hutufungulia mlango wa rehema na uweza wake Mola, akisharidhia sala zetu kilicho salia ni sisi kuenenda kwa utiifu na uadilifu. Naye pasi na wasiwasi atazidi kudumisha Uwepo wake maishani mwetu, na hii ni bakara isiyo na kifani; Ibrahimu ka’elimishwa vile na Musa katambua ndivyo, (MWA. 15:1; KUT. 33: 15-16). Je, kwetu sisi twatarajia tuwe tofauti na bado tuuone ushindi wake ukitutangulia? Abadan katani, nakuhakikishieni haijawahi na haitawahi fanyika wala tusijidanganye itatendeka kwetu sisi. Kwani tubora kuliko Ibrahimu swahiba yake Mwenyezi Mungu au Nabii Musa aliyenena naye uso kwa uso? Haitupasi sisi zaidi Ee, wapendwa kulishika na kulitegemea Neno Lake, maana kwetu sisi kupitia dhabihu takatifu ya Mwana wake wa Pekee atuhakikishia ahadi zake zote ni “Ndio na Amina,” (2KOR. 1:18-19).

 

Natuzidi wateule wa Bwana, tuzidi kutembea katika njia hii ambayo tumeikanyaga, kamwe hatutajuta sawa na hao ndugu zetu walio tutangulia. Nikitamatisha, kwa mfano wake Utimilifu wa Mungu, huyo Mwamba wa Milele, (MAT. 7:24-27),hapa anatutofautishia mwenye hekima na  mpambavu ni nani. Na kudhihirika kwao kwaja wakati masumbuko na majanga yanapowakabili. Hebu tafakari: Je, ni yupi nyumae atapaaza sauti na kusema, Bwana akatia wimbo mpya kinywani mwangu, ndio sifa zake Mungu wetu? Isitoshe, nani bado itakapohitajika ataweza kusimama tisti mbele za waovu na wanaokufuru Jina lake Mtakatifu wa Watakatifu akiwa na ushuhuda utakao wafanya wengi kuogopa na kumtumaini Bwana? 

No comments:

Post a Comment