HAMMO GIZANI: MMEKUWA WANA WA NURU NA WANA WA MCHANA (SURA YA 2)
Neema
na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
Mungu mwenye enzi ya milele na
milele, tunakutukuza na kukushukuru kwa wema na rehema zako maishani mwetu. Maana,
Ewe ndiwe Muumba wa vyote, iwe ni juu Mbinguni, hapa Duniani na Ulimwenguni
mzima. Vyote vinavyoonekana na visivyoonekana viko chini ya uweza wako kwa kuwa
vyote vinakuhitaji na kukutegemea Ewe, Mungu, Muumba na Muumbuaji. Isitoshe, hakuna
kinacho weza kufananishwa nawe, kwa kuwa hauhitaji chotote au kumtegemea ye
yote. Hauna mwanzo wala mwisho bali mwanzo na mwisho ni kazi yako Ewe, Alfa na
Omega. Daima uhimidiwe na utukuzwe. Amin.
Tumejaliwa wiki nyingine na Bwana
wetu, kwa hiyo tusilegee katika ibada na kumtumikia kwa mali zetu zote na
katika kila hali, maana vyote tulivyo navyo ni vyake Yeye Karima, (RUM.
11:33-36). Kwanza tutarejelea somo la wiki jana kimukhtasari; tuwezaona umuhimu
wa maombi na kusoma Biblia Takatifu kwa maisha ya mwanadamu na zaidi kwetu sisi
Wakristo. Vile vile kuhakikisha kuwa kwa njia hii watakatifu wa kale walipata
kujua mawazo ya Mola, na kuwezeshwa kutenda yaliyo sawa na mapenzi yake katika
zamani zao. Sawa sawa na hayo tulitambua kwamba, hakuna njia mbadala kwetu sisi
watakatifu wa zamani hizi ikiwa twataka kutenda mapenzi ya Mola wetu na
kuhesabiwa haki mbele zake, (2TIM. 2:14-15; SEF. 2:3). Basi, enyi wapendwa
katika Kristo Yesu, tuzidi jibidiisha katika njia hii tukiwakumbuka watakatifu
wote aidha wawe wa madhehebu yetu au la, kwani sote tu viungo vya mwili mmoja
(Kanisa) ambaye kichwa chake ni Kristo Yesu, (KOL. 1:13-18; 1KOR. 1:10-13).
Nasisitiza hivi kwa kuwa muda uliopo
ni mfupi mno; saa ya kuja kwake Bw. Yesu kulichukua Kanisa lake imewadia! Walakini,
Mkombozi wetu hatakuja bila kutuarifu na kutufanya tuwe tayari kwa ujio wake, sawa
na enzi za kale Mungu alipotaka kutenda jambo kwanza aliwafahamisha watu wake.
Aliwainua manabii kati yao na kuwapa karama na vipawa vya kila aina ili kuwafunza
na kuwahubiria watu; wanyoshe njia zao na kuacha dhambi. Wajiweke tayari kwa
ujio wa Mungu, aidha kwa rehema au hukumu. Mimi na wewe mpendwa hili ndilo
jukumu letu katika kizazi hiki, tujitakase ili tupate kukubalika mbele za Mungu
kwa maneno yetu pamoja na mwenendo wetu tuwafae wengi kwa kuwakumbusha
utakatifu na utukufu wa Mungu. Wengi wakapate kuutazama mfano wetu na kumrudia
Mungu Baba na kujengeka katika imani, huku tukiitazamia SIKU YA BWANA, (YOE.
2:17; 1PET. 2:9-10).
Wapendwa, msichukulie ni tashtiti
wala kuchoshwa nakuhimiza kwangu; si ati sifahamu kuwa mambo haya ni ya msingi
katika jumuiya nzima ya Wakristo, ila nawapeni tahadhari ya kwamba kila nabii
aliyeitabiri SIKU YA BWANA alishinikiza kuwa yaja upesi! Sasa itakuwaje kwetu
sisi ambao dalili zote zaonyesha kuwa enzi hii tuishio ndiyo waliotabiri
kuihusu? Inatulazimu sote tunaompenda Kristo Yesu kwa nia moja tushirikiane
kuimarisha mwili wa Kristo ko kote tuliko; nyumbani, shuleni, hata kazini,
(2KOR. 5:1-10). Hasa, yatupasa kutambua yale Mungu Baba ameyaweka tayari kwa
ajili ya watu wake katika kipindi hiki, ili tujihami vilivyo na yatakayo ikuta dunia hii hivi
karibuni kama tulivyoona katika masomo yaliyotangulia. Pia katika hayo
tuliyosoma tulitambua zama hizi za leo za fanana zamani zile za Ufalme wa Yuda,
kabla Mfalme Nebukadneza kuuvamia na kuupiga Ufalme ule kwa upanga. Na jinsi
Mungu alivyofanya juu chini kupitia manabii wake ili awanusuru watu wake lakini
wao walizidi kumkaidi hadi hukumu yake Mungu ilipowafikia sawa na yale
aliyoyanena kwa vinywa vya manabii wake.
Kipindi hicho cha Ufalme wa Yuda kilichofanana
na enzi hii yetu kilianza na umiliki wa Mfalme Manase. Mfalme huyu, aliijaza Nchi
ya Yuda damu isiyo na hatia na kuwapotosha watu wa Mungu kwa kutenda kila aina
ya maouvu mpaka kuleta sanamu hekaluni na kumtoa mwanawe kafara kwa hiyo sanamu
papo hapo hekaluni!....... Eeh, sitayarudia yote tuliyozungumzia, ila nataka
kuwakumbusheni katika kipindi hicho kuna Mfalme mmoja aliye tenda tofauti na
matendo ya wenzake, enhe, si mwingine ni Mfalme Yosia. Yeye ndiye aliye haribu
sanamu hizo za Mfalme Manase, na kutoa amri Hekalu likarabatiwe na ibada pamoja
na matoleo ya kila siku ya rejeshwe kama hapo awali. Kupitia juhudi zake Yuda
ikapata muamko mkuu wa imani na kumrudia Mungu wa Israeli. Kwa kifupi nasema
hivi, sawa na vile tulivyoona enzi hiyo ya kale ikiwa kioo cha enzi hii ya leo,
hivyo ndivyo twatarajia kutatendeka, (2FAL. 22-23).
Mungu atamwinua mtu atakaye tumika kuleta
uamusho katika Kanisa lake kabla hajatekeleza hukumu yake duniani. Tofauti
itakayokuwepo ni kuwa sote tutakaokuwa tumesafisha “nguo zetu” na kuwa safi
tutashiriki katika uamusho huo. Uamusho huu ndio utatimiza kwa utimilifu neno
lile alilolinena Nabii Yoeli kuhusu Roho wa Mungu kumiminwa juu ya wote wenye
mwili kabla ya SIKU YA BWANA, (YOE. 2:28-32). Kanisa tujiwekeni tayari, Mungu
anakusudia kutenda mambo makuu katika Mwili wa Kristo na kisha autumie kwa
uweza na utukufu kuhubiri Ufalme wake kabla haja ihukumu dunia hii kwa moto.
No comments:
Post a Comment