Sauti za uasi zimekuwepo
Sauti za uasi zimekuwepo, msijitie
bashasha zenu sio za kwanza
Tazameni uasi huu wa kipepo, magauni
na surwali ndo wameongeza
Msidanganyike ati ni maedeleo,
kumbukeni Edeni baada yao kudanganywa
Mungu alishutumiwa na kufanywa
chukizo, ati asingelipenda wawe kama Mola
Sauti za uasi zimekuwepo, msijitie
bashasha zenu sio za kwanza
Maendeleo mmeifanya nduano, mithili
Nimrodi Babeli kujenga
Vyeti na mashahada mmejaza mifuko,
waja kuwatisheni ati hekima imewakolea
Wale dhaifu shabaha ya venu vitisho,
ila waadilifu twajua kingo za wenu
ujanja
Sauti za uasi zimekuwepo, msijitie
bashasha zenu sio za kwanza
Babenyu ni yule mwongo, shaitwani
mwingi wa kibri na shutma
Kabla ya ulimwengu kuwepo, hatiani
Mola kampata
Kazua uzushi kijitakia cheo, enzi
aimiliki kana kwamba ndiye Mumba
Sauti za uasi zimekuwepo, msijitie
bashasha zenu sio za kwanza
Uhuru wa kujieleza twajua upo,
msifyate midomo twa wahimiza
Ukombozi pia upo, katu Injili
hamwezi ilemaza
Japo giza kawa totoro, nuru ya
Injili kote itaangaza
Sauti za uasi zimekuwepo, msijitie
bashasha zenu sio za kwanza
Matusi mwazidisha kila uchao, ila
hamtafanikiwa imani kudhalalisha
Hadhara tahadhari yao maelezo, maana
mwana wa nyoka daima ni nyoka
Uasi kweli ni uozo wala sio
maendeleo , ila laana sitowaombea bali neema inayookoa