Sunday, 4 May 2014

HAKUNA MUNGU!

HAKUNA MUNGU: Dhana hii si mpya imekuwepo tangu jadi! Zaburi (Psalms), 14: 1


Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.


Kwa kweli sijui nianzie wapi! Kawaida sipendi kujihusisha na michakato ambayo ni ovyo. Yaani haina msingi wala lengo lolote lile la manufaa katika jamii ila kueneza upambavu na upotovu! Bali, nakuulizeni, je, ni jambo ndogo kufanya dhihaka na kuchukulia upuzi ishara zote ambazo bayana zinatudhihirishia kuwa Mungu yupo? Nakuulizeni tena; je, ni jambo ndogo?


Ati, limbukeni wanashikana kuunda kikundi ambacho msingi na shabaha yake nikueneza dhana hii hii pumbavu na potovu eti, HAKUNA MUNGU! Ewe, Mwingi wa fadhila tafadhali tuepushe mbali na shari zako. Jamani, kwani ni upeo upi huu au ngazi gani hii ya elimu, ambayo hawa chipukizi wamezamia? Maanake hapa ni dhahiri kuwa wanahitajia maelezo mbadala.   


Uzushi huu, una malengo maalum! Usishangae baada ya muda tukapata kusikia kuhusu ufadhili toka kwa makundi fulani ya ughaibuni na mialiko yakuturai tukahudhurie vikao vilivyo andaliwa kwa mbwembwe nyingi na gharama kuu. Nia ikiwa sio nyingine, bali, kuwatega na kuwanasa walio wepesi kiakili na wale ambao baado hawajafanya azma madhubuti kufuata muundo fulani katika maisha yao. Itakuwaje basi; tufyate midomo ama tufunge macho pamoja na kuziba masikio kwa dai ati, hii ni karne ambayo uhuru wakujieleza upo, umetambulika na kuheshimika na wote! Mmmh! Kama huo ndo mwelekeo basi haina budi kuujibu mchakato huu kwa mujibu wa kanuni hiyo hiyo.  


Kwa neema na kudura zake Mwenyezi, tutaweza kuwaopoa toka upambavu huu uliokithiri na kuwarejesheni katika akili razini na mtazamo wa maisha uliosawa na hali halisi ya mambo. Hapa naigusia kanuni moja kuu, inayokubalika mia-fil-mia katika fani zote za utafiti na uchanganuzi wa kielimu. Kanuni yaelezea kwamba, Kazi iwayo yoyote ile ya kiufundi lazima iwe imefanywa kwa akili na kwa ajili ya lengo mahususi. Nitataja mambo mawili pekee, baadhi ya mengi yaliyoko ili kufafanua kanuni hii;



  • Mandhari na uhai hapa Duniani: Hivi sasa hakuna awezaye kupinga uhodari uliopo katika mpangilio wa maumbile; milima, miti, visiwa, bahari, jangwa, au nyika. Vyote kwa mujibu wa wanamazingira kama hayati Prof. Mama Wangari Mathaai, ni muhimu na huchangia si haba katika kuwepo kwa uhai hapa duniani. Maanake kila kiumbe kina umuhimu wake, manufaa yake na lengo maalum la kuwepo. Je, tunapo tenda kinyume na kuhujumu mpangilio wa maumbile? hasara iliyoje ambayo hutupata, kama vile ukataji miti kiholela………………    

  •  Mpangilio wa sayari toka Zebaki (Mercury) hadi Utaridi (Pluto): Kila moja ya sayari hizi huwa na majira yake na mzingo wake maalum unao zunguka Jua; haya hutendeka pasipo hata sayari moja kukosea njia au kupitwa na masika yake. Kama unamiliki Saa ya mkononi fungua nyuma ushuhudie majira ya saa yako yanavozunguka. Je, utasema ufundi huo unaoutazama ulijiunda pasipo fundi wa aina yeyote?

     

Tazama tu, vile ilivyo rahisi kudhibitisha ustadhi na ustadi wa Mwenyezi katika kazi alizozifanya kwa hekima na uweza mkuu!

 

 

Natumhimidi Yeye aliye juu, na kumsifu na kumheshimu Yeye aishiye milele; kwa maana enzi na mamlaka Yake ni ya milele hadi milele na matendo Yake yote ni kweli, na njia Zake ni za adili. Na atukuzwe Bw. Yesu Kristo, Utimilifu wake Mungu wa Kweli ulimwenguni kote. Amin.

 

No comments:

Post a Comment