Sunday, 11 May 2014

MEZA YA BWANA




Meza ya Bwana: Madhumuni ya itikadi hii kuwepo katika familia teule ya Wakristo.

Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

Kabla ya kuzama katika mada yetu ya leo, najua vema kuwa Wakristo tuko na itikadi zetu tofauti kulingana na madhehebu tunayoshiriki. Lakini, kati ya itikadi hizo kunazo kadhaa ambazo hutimizwa na Mwili wote wa Kristo yaani Kanisa, baadhi ikiwa: Ubatizo; Kukiri imani ya Mitume (Apostle’s Creed); Kushiriki Meza ya Bwana na Ndoa.

Kama tujuavyo kila umma, taifa, muungano, kampuni au dini huwa na desturi na itikadi zake maalum. Vivyo hivyo, pia kwetu sisi tunao kiri imani ya Ukristo zipo itikadi ama ukipenda Sakramenti teule ambazo lazima kila Mkristo atimize kwa njia moja au nyingine; Sakramenti hizi bila shaka ni muhimu katika malezi, ukuaji na uimarishwaji kiimani na maishani.

Basi, bila kuchelewa tuingilieni mada yetu ya leo. Kisa na maana,  picha hiyo ya dharau mlioweka katika ukuta wenu wa facebook Mmmh! Nakuulizeni picha hii (cover photo) ndo yaonyesha uhuru wakujieleza? Si uchokozi huo! Si matusi hayo! Kama kweli hakuna Mungu, mbona mnawashwa na shughuli zake? Mbona mna kufuru (blaspheme)?

Enyi mlio shadidi wa cheche za matusi na majitapo, nitawaelezeni nini maanake kushiriki Meza ya Bwana. Kwa kifupi, kushiriki meza ya Bwana, nikuadhimisha peupe kifo cha Bwana Yesu Kristo msalabani kwa ajili ya dhambi zetu Binadamu. Fauka ya hayo, inahuisha kiroho na huleta faraja na baraka zisizoweza kuelezeka. Na, je, kuna madhumuni mengine ya itikadi hii kuwepo katika familia teule ya Wakristo? Kwa hikika ndio, na yafuatayo ni baadhi ya Maandiko yatakayo tupatia mwongozo mwafaka kujadili itikadi hii kwa upana zaidi;


Agano Jipya: (MAT. 26:26-28; MK. 14:22-24; LK. 22:14-20).Tokea ibra ya kuzaliwa kwake Kristo, maisha yake, matendo yake hata kusulubiwa na kufufuka kwake na kuja kwake tena; matukio yote haya huwa yamefungamana na chakula hiki. Kwa maelezo ya maandiko hayo ulioyasoma, Yesu anaweka wazi kabisa, kwamba chakula hiki japo kuwa ni cha kawaida (Mkate na Divai) kwa wakati ule na fuatia hapo, kulingana na mfumo anaoasisi, chakula kile kikiandaliwa vile kitakuwa cha kipekee. Sababu yake kuu ikiwa ndo hati ya Agano Jipya, pia ikiwa sharti itikadi hii itimizwe milele.



Hakika Ya Ufufuo: Yohana (YN.) 6:52-54. Hapa Bw. Yesu akiwa katika hulka yake ya kuhubiri Ufalme wa Mungu, wanaomskiza wanaanza kushindana kwa kutoelewa maneno yake. Lakini, tazama ujasiri ulioje na hakika yake, kwa yale anayowaeleza! Labda walidhani ameteguka ulimi, maana ulimi hauna mfupa au sivyo? La, hasha! Amin, amin, kaisema mara mbili ili kusisitiza yanayomtoka kinywani ni ukweli mtupu pasipo ati-ati wala wahaka wowote ule. Ni sharti, ule mwili wake na unywe damu yake ili uwe na uzima ndani yako. Nayo siku ya mwisho itakapofika ufufuo utakuwa haki yako.


Shibe Toka Mbinguni: (YN. 6:55-59). Huku mashindano yakiendelea katika umati ule, Bw. Yesu; mwalimu shadidi, anatumia fursa hiyo ya sintofahamu kufafanua maneno yake. Wayahudi wale walokuwa pale mbele zake, wanafahamu vema miujiza na ishara za Mungu na jinsi zilivyo ambatana na mababa zao walipokombolewa toka utumwa huko Misri, ususan, mkate ulioshuka toka mbinguni wakiwa njanguani. Bali, Bw. Yesu, anasema yeye ndo chakula cha kweli tofauti na mkate ule, maana walokula mkate ule baado walikufa. Lakini, “aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake……..kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi.” Kuna Baraka gani zaidi ya kupokezwa uzima wa milele na uwepo wa Mungu Baba kuwa nawe daima?


Kuja kwa Ufalme wa Mungu: (LK. 22:14-20). Kwanza natutazame mapenzi na ustarabu wake Bw. Yesu; ijapokuwa anakusudia mateso yakutamausha, shauku na fahari yake kubwa ipo kwa wale wandani wake! Ili kuwaondolea huzuni kabla na kuifanya imani yao dhabiti anapanga maandalizi haya murwa, licha ya tabu na mauti inayomchungulia mlangoni! Kusudi analolipa kipaumbele ni kuwapa ukakamavu na kuhifadhi imani ya wale maswahiba wake. Ili mateso yatakapoanza wasijeona kana kwamba mambo yamemzidi kwa lolote lile, la hasha! Bali madhila yatakayo mkuta  ni sambamba na mpangilio wa Mungu Baba, ili Ufalme wake ukaweze kuja na wote watakao timiza itikadi hii kwa mujibu wa imani, wawe warithi wa Ufalme huo tukufu na takatifu.


Kuungama kifo chake hadi atakaporudi tena: (1KOR. 11:23-26). “Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo,” hivi ndivyo Mtume Paulo anavyoanza aya hii ya 11. Madhumuni yake nikuhakikisha Wakriso wanafahamu hatua zake Bw. Yesu na kuzifuata timilifu. Katika swala la kushiriki Chakula hiki hatua ile ile Kristo alokuwa nayo ni kutilia mkazo dhana ambayo hudhihirika dhahiri shahiri kwa wote kila wakati Wakristo wanapotimiza itikadi hii; dhana hii sio nyingine, ila kuungama kifo chake Bw. Yesu, kwa ajili ya dhambi na utarajio ulioko moyoni mwa washirika kuwa atarudi tena.


    Mwili Mmoja: 1Wakorintho (1KOR.) 10:16-17. Mtume Paulo, kwenye waraka huu anajishughulisha kurekebisha mambo kadha yalokuwa yakitendwa kinyume na tabia, desturi na itikadi za Ukristo. Anapotua katika swala nzima linalo husu Meza ya Bwana, anaelezea kinaganaga nini kiini cha ushirika ule, “kama vile mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.” Pasipo kutilia shaka anamaanisha mwili wa Kristo, kama alivyo tangulia kwa kuuliza, ni kikombe kipi tunachobariki na ni mkate upi tuaoumega? Kikombe sio kingine ila kile kilicho jaa damu ya Kristo na mkate sio mwengine ila mwili wa Kristo. Kwa ushirika huu aila yake Mungu dunia nzima hufanyika kuwa mwili mmoja.


Hukumu: (1KOR. 11:27-32). Hapa Mtume anawatahadharisha washirika wale tokana na tabia zao mbovu zinazoshushia Meza ya Bwana hadhi na heshima inayostahiki. Kwa kuja na kujishibisha matonge ya mikate na kubugia vikombe mpaka wakalewa chakari, ilhali wenzao wabaki njaa! Zaidi, utovu huu wa nidhamu ambao unakaidi heshima na utakatifu wa Meza ya Bwana anaushirikisha na wale wasio weza kuupambanua Mwili wa Kristo. Maanake yeyote ule ambaye ana fahamu Kristo ni nani na kazi alioifanya hawezi katu kutenda vile. La kusononesha ni kuwa onyo hii pakubwa inalenga Wakristo! Lakini dhamani yake ni kuwa lengo lake ni kutuepusha na hukumu itakayopata dunia hii. Vile vile, onyo hii inawalenga wasioamini, maana, pasipo imani huwezi pambanua Kristo ni nani na umuhimu wa kazi alioifanya!

 

Daima, Wakristo tumshukuru Mwenyezi, kwa Agano Jipya. Maana, kwa wingi wa mapenzi, wema na fadhila zake alitukomboa tokana na adhabu ya dunia hii. Ushirika huu kwetu ni onyesho la imani yetu, kwake kipenzi chetu Bw. Yesu Kristo, kwa kutudhamini sisi zaidi ya uhai wake mwenyewe. Amin.


 

No comments:

Post a Comment