Sunday, 27 July 2014

IMANI YA KWELI NI KUFAHAMU NA KUTENDA NENO LAKE (SURA 2)



Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

 


Ahimidiwe, Mungu Baba, juu mbinguni, hapa duniani na ulimwenguni kote. Kwa kudura zake ametuwezesha kupatana tena katika ukurasa huu, ili tukaweze kuzidi kuangazia yanayotukabili siku baada ya siku kwa minajili ya kufahamu nyakati tunazoishi. Tukidurusu kwa ufupi; wiki jana tuelekezea kurunzi kadhia ambazo zimekuwa zikiendelea hapa nchini na kuona jinsi Mwenyezi anavyotilia manani maisha yetu, na kutuepusha na uharibifu mara tulipoinua sauti zetu na kumlilia. Ahsante, zetu kwa fadhila zako Baba wa mbinguni. Walakini tusiache kufunga na kuomba hadi nchi yote itakapotulia tuli. Leo hii tutaendeleza mchakato wetu wa “imani ya kweli,” huku tukilenga kujinasua tokana na kasumba ya kutumainia mali.

 

Mwongozo wetu wa maisha kama desturi na itikadi ya Kikristo hutoka kwa Neno Tukufu la Muumba wa vyote:- Biblia Takatifu. Zaburi 49, sawa na chapisho la wiki ilopita ndio inatupa mwelekeo ufaao kwa mchakato huu. Wapendwa, sote twajua kuwa mali au utajiri una ushawishi mkuu tena wengi hushindwa kustahimili mshawasha wake kiasi cha kupoteza nafasi zao katika makao ya milele, MT. 19:16-24. Kunena hivi haimanishi tuchukulie aliyejari sawa na mtu aliyepotea, asilani! Utajiri ni Baraka toka kwake Karima anyegawia wote kwa hekima zake. Bali kufanya mali kuwa tegemeo na tumaini hapo ndipo mja hupotoka, LK. 12:13-21. Fika hapa najua wengi watasema mambo haya twajua vema. Nami nitawaulizeni kweli mwafahamu?

 

Kuuliza vile si kejeli bali nikutoa ilani ya mambo yanayotusibu! Wakristo hebu tujirudi wenyewe natuone jinsi Mwili wa Kristo (Kanisa) ulivyo adhirika kwa kuegemea mali, vilevile, serikali na asasi za utawala. Pakubwa mali na utajiri umefanywa chanzo cha kuheshimika na kukubalika katika jamii. Nao wenye mali wamekuwa ndio washauri wakutamanika na kuaminika, bora unacho utategewa sikio na kulimbikiziwa sifa sufufu. Fauka ya hayo utakwezwa na kufanywa kielelezo cha wengi licha ya utovu wa maadili na hata zaidi kukosa imani! Wahenga kamwe hawakukosea waliponena mavi ya tajiri hayanuki.a

 

Mambo haya kama tujuavyo yamechangia changamoto na taabu si haba katika Kanisa pamoja na utawala wa nchi; ushawishi mkubwa unaotukabili ukitokana na nchi tajiri duniani na zenye uwezo. Sio siri kuwa nchi hizi zimejizatiti kueneza na kufadhili upotovu na uovu wa kila aina duniani kote. Ole, wetu sisi wanyonge tutakapo acha mwongozo wa Biblia Takatifu na kushika mafunzo yao: Talaka; Usenge na Usagaji; Uafyaji Mimba; Uasi Mungu, ni baadhi ya uchafu unaopaliliwa duniani na hao matajiri wenye uwezo, na kubatizwa maisha ya kisasa. Bali wakristo tusichoke kuenenda katika uvumilivu na unyenyekevu mwishowe Mungu wetu atatufariji, MT. 5:1-13; LK. 6:20-26. Ijapokuwa  tutafinyika tunahakika kwa kinywa cha Kristo mwisho wetu ni mwema, tofauti na hawa wanaoupotosha ulimwengu, hao tusiwaogope wala kuzitamani njia zao, ZAB. 49:16-20.


 

Mbarikiwa ni ewe Mkristo unayejiwekea akiba mbinguni kwa matendo ya adili pamoja na kukesha na kuomba huku ukimtarajia Mkombozi, MT. 6:19-21; Lk. 19:11-27. Mwenyezi, aridhie kutunasua na uchu ya mali, bali atuzidishie uwezo na kaida ya kuenenda tukiwa imara katika hatua zetu tukifuata nyayo zake daima. Pamoja nakutenda haya tukumbukeni viongozi wetu wa Kanisa na Taifa, tuwapeane kwake Mchungaji Mwema ili awaongoze kule kwema kwa hekima na uweza. Zaidi tukumbukeni, hata katika taabu na majaribu ni vema zaidi kumhimidi Mungu kuliko mwanadamu, ZAB. 49:5-15.   

 



Natumhimidi Yeye aliye juu, na kumsifu na kumheshimu Yeye aishiye milele; kwa maana enzi na mamlaka Yake ni ya milele hadi milele na matendo Yake yote ni kweli, na njia Zake ni za adili. Na atukuzwe Bw. Yesu Kristo, Utimilifu wake Mungu wa Kweli ulimwenguni kote. Amin.

Sunday, 20 July 2014

UZIMA WA MTU HAUTEGEMEI UTAJIRI WA MALI

 

Sikieni haya, enyi mataifa yote; Sikilizeni, ninyi nyote mnaokaa duniani.

 

Watu wakuu na watu wadogo wote pia, Tajiri na maskini wote pamoja. 

 

Kinywa changu kitanena hekima, Na fikira za moyo wangu zitakuwa za busara. 

 

Nitatega sikio langu nisikie mithali, Na kufumbua fumbo langu kwa kinubi 

 

Kwa nini niogope siku za uovu, Ubaya ukinizunguka miguuni pangu? 

 

Wa hao wanaozitumainia mali zao, Na kujisifia wingi wa utajiri wao; 

 

Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake, Wala kumpa Mungu fidia kwa ajili yake, 

 

(Maana fidia ya nafsi zao ina gharama, Wala hana budi kuiacha hata milele;)

ili aishi sikuzote asilione kaburi. 

 

Naam, ataliona, hata wenye hekima hufa; Mpumbavu na mjinga hupotea pamoja, Na kuwaachia wengine mali zao. 

 

Makaburi ni nyumba zao hata milele, Maskani zao vizazi hata vizazi. Hao waliotaja mashamba yao Kwa majina yao wenyewe. 

 

Lakini mwanadamu hadumu katika heshima, Bali amefanana na wanyama wapoteao. 

 

Hiyo ndiyo njia yao, ujinga wao, Nao walioko baada yao huyaridhia maneno yao.

 

Kama kondoo wamewekwa kwenda kuzimu, Na mauti itawachunga; Watu wanyofu watawamiliki asubuhi; Umbo lao litachakaa, kao lao ni kuzimu. 

 

Bali Mungu atanikomboa nafsi yangu, Atanitoa mkononi mwa kuzimu, maana atanikaribisha. 

 

Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi. 

 

Maana atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata. 

 

Ajapojibariki nafsi yake alipokuwa hai, Na watu watakusifu ukijitendea mema, 

 

Atakwenda kwenye kizazi cha baba zake Hawataona nuru hata milele. 

 

Mwanadamu mwenye heshima, iwapo hana akili, Amefanana na wanyama wapoteao. 

 

 

Zaburi 49

Sunday, 13 July 2014

IMANI YA KWELI NI KUFAHAMU NA KUTENDA NENO LAKE (SURA 1)



Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

   

Enyi wateule zake Haki, Ewe, Mwenye uweza wote, juu mbinguni, hapa duniani, chini kuzimu na ulimwenguni kote, kheri na fadhila zizidi kuwatangulia toka kwake Masihi wa Mungu uyo huyo aliye Ufufuo na uzima. Hususan katika kipindi hiki ambacho sote tunang’amua kuwa kimejaa changamoto tele nchini na dunia nzima. Tukichukulia hatua toka chapisho lililotangulia; Zaburi 40, nivema kutangulia kumshukuru Mungu, bila kuchelea kwa maana ametujalia neema zake ambazo ni za milele. Hebu tutafakari kwa kina yale yamekuwa yakitokea nchini; uvamizi, mauaji ya kiholela, milipuko na mashambulizi ya kigaidi, uhasama wa kisiasa na kwa ujumla utulivu kutupotea kwa kila hali! Kijumla twaweza sema, hali ya taharuki, majonzi na kiwewe ilikuwa imeigubiga mipaka yote ya taifa letu!

 

Licha ya giza kukaa kama ingetufunika, ghafla nuru ya amani ikachomoza! Swali la msingi litupasalo kujiuliza ususan sisi Wakristo ni:- nikipi hasa ambacho kilitendwa kwa mkono wa mwanadamu ili utulivu uanze kurejea? kama kawaida hapa wengi watatapatapa kwa visingizio vya kila aina na maelezo marefu yaliyosheheni misamiati utadhani ni mashindano yakutwikwa taji la kujieleza kwa ufasaha kwa Kimombo. Bali kando na sokomoko hizo zote aliye na macho hambiwi tazama, maanake, bila shaka ahsanta, zote nikwake Mwingi wa Rehema. Yeye, Rahmani mwingi wa Huruma ndiye katupandisha toka shimo la uharibifu na toka udongo wa utelezi. Enhe! Si kwa mkono wa yeyote ule ila kwa uweza wake Mungu wa Kweli. Yeye karidhia kutuepusha na uharibifu kwa kusikia kilio cha wanawe wateule; Wakristo. Bila kusitasita, itambulike bayana kuwa ni maombi ya Wakristo, kwa kufunga na kuombea taifa hili huku tukimlilia na kumgoja Mungu Baba kwa uvumilivu ndiyo yamefanya haya. (ZAB. 133; MAT. 18:18-20).

 

Wapendwa, tazameni makuu yanayotendeka Mwili wa Kristo; Kanisa, linapoamua kuenenda kwa umoja na kwa ujasiri wa imani! Kila wakati tunapochukua hatua sawa na Neno Lake Muumba mambo hutengenea sambamba na ahadi zake. Hivi ni kusema kwamba kama kweli tutamtegemea kwa kutimiza mapenzi yake maishani mwetu kila siku basi hatuna budi kuuona uweza wake mkuu ukitushindania kwa jambo lolote lile, (KUT. 6:6-7). Uhakika wa mambo ndio huo, na kama tunatambua hivi, basi nini hasa huwa kinatukwaza tusiendelee na moyo huo wa umoja na maombi? Na nilipi la busara kutenda ilitujiepushe na majanga kama haya kutufika tena? Majibu ya kuridhisha na ushauri nasaha hautopatikana kwengine ila  kwa Neno lake. Ni hapa tu, katika Biblia Takatifu pekee ndipo tiba ya magonjwa na matatizo yote yapo. Basi nakuulizeni kwa nini kujitaabisha kwa kuzurura huku na huko? Badala yake tujichoshe na kuvunjika nyoyo huku tukiwa wakavu, tukichekwa hata kudharauliwa na hao mahasidi wa imani yetu!

 

(ISA. 9:6). Sio bora zaidi tulivyotangulia kufululiza kusimama mwambani pahala ambapo hatua zetu ziliimarishwa kwa ajili ya dua. Hivi sasa nani hana wimbo midomoni akielezea utulivu ulorejea? Kama atupeavyo Jua na Mvua, wema kwa wabaya, vilevile amani hutufikishia sote. Wapendwa, nafanya kusisitiza ili tusikizane, maombi ndio hutufungulia mlango wa rehema na uweza wake Mola, akisharidhia sala zetu kilicho salia ni sisi kuenenda kwa utiifu na uadilifu. Naye pasi na wasiwasi atazidi kudumisha Uwepo wake maishani mwetu, na hii ni bakara isiyo na kifani; Ibrahimu ka’elimishwa vile na Musa katambua ndivyo, (MWA. 15:1; KUT. 33: 15-16). Je, kwetu sisi twatarajia tuwe tofauti na bado tuuone ushindi wake ukitutangulia? Abadan katani, nakuhakikishieni haijawahi na haitawahi fanyika wala tusijidanganye itatendeka kwetu sisi. Kwani tubora kuliko Ibrahimu swahiba yake Mwenyezi Mungu au Nabii Musa aliyenena naye uso kwa uso? Haitupasi sisi zaidi Ee, wapendwa kulishika na kulitegemea Neno Lake, maana kwetu sisi kupitia dhabihu takatifu ya Mwana wake wa Pekee atuhakikishia ahadi zake zote ni “Ndio na Amina,” (2KOR. 1:18-19).

 

Natuzidi wateule wa Bwana, tuzidi kutembea katika njia hii ambayo tumeikanyaga, kamwe hatutajuta sawa na hao ndugu zetu walio tutangulia. Nikitamatisha, kwa mfano wake Utimilifu wa Mungu, huyo Mwamba wa Milele, (MAT. 7:24-27),hapa anatutofautishia mwenye hekima na  mpambavu ni nani. Na kudhihirika kwao kwaja wakati masumbuko na majanga yanapowakabili. Hebu tafakari: Je, ni yupi nyumae atapaaza sauti na kusema, Bwana akatia wimbo mpya kinywani mwangu, ndio sifa zake Mungu wetu? Isitoshe, nani bado itakapohitajika ataweza kusimama tisti mbele za waovu na wanaokufuru Jina lake Mtakatifu wa Watakatifu akiwa na ushuhuda utakao wafanya wengi kuogopa na kumtumaini Bwana? 

Sunday, 6 July 2014

HERI ALIYEMFANYA BWANA KUWA TUMAINI LAKE



 

Nalimngoja Bwana kwa subira, Akaniinamia akakisikia kilio changu.



Akanipandisha toka shimo la uharibifu, Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua zangu.



Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, Nao watamtumaini Bwana



Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake, Wala hakuwaelekea wenye kiburi, Wala hao wanaogeukia uongo.



Ee Bwana, Mungu wangu, umefanya kwa wingi Miujiza yako na mawazo yako kwetu; Hakuna awezaye kufananishwa nawe; Kama ningependa kuyatangaza na kuyahubiri, Ni mengi sana hayahesabiki.



Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, Masikio yangu umeyazibua, Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.



Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (Katika gombo la chuo nimeandikiwa,)



Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.



Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa. Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua.



Sikusitiri haki yako moyoni mwangu; Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako. Sikuficha fadhili zako wala kweli yako Katika kusanyiko kubwa.



Nawe, Bwana, usinizuilie rehema zako, Fadhili zako na kweli yako na zinihifadhi daima.



Kwa maana mabaya yasiyohesabika Yamenizunguka mimi. Maovu yangu yamenipata, Wala siwezi kuona. Yamezidi kuliko nywele za kichwa changu, Na moyo wangu umeniacha.



Ee Bwana, uwe radhi kuniokoa, Ee Bwana, unisaidie hima.



Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu.



Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe!



Washangilie, wakufurahie, Wote wakutafutao. Waupendao wokovu wako Waseme daima, Atukuzwe Bwana.



Nami ni maskini na mhitaji, Bwana atanitunza. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, Ee Mungu wangu, usikawie.  (Amin)

Zaburi 40