Sunday, 24 August 2014

TUNU YA MOYO WANGU



TUNU YA MOYO WANGU
 

Nitanena bila sitara pasi na kuficha, utengano kuufisha upatano ututhibitikie,

Naam, mawazo ya moyo wangu sitakuficha, siri ya mtima wangu nikufunulie,

Laazizi hakika kama we'e sina hata pacha, mboni la jicho langu sogea unigeukie,

Ewe tunu ya moyo wangu sogea, tusemezane kipenzi changu.

 

 

 

Kibri na purukushani hazitokufaidi, sichukulie nitashtiti mwenyewe tasadikia,

Takufukizia shauri langu kama udi, ingawa shubiri nafsini tapenya shalikia,

Ungelirekebisha kamwe singekuridi, na katu sitochoka mema kukutakia,

Ewe tunu ya moyo wangu rekebisha, ufaidike kipenzi changu.

 

 

 

Uhodari wako nautambua sawa na udhaifu wako, si mie kakufanya jinsi ulivyo,

Kwa udongo nikaifanya misingi yako, kindakindaki nakufahamu kwa hivyo,

Ila tafakari fahari yote ya maisha yako, yote hudumu kama umande ukaavyo,

Ewe tunu ya moyo wangu tafakari, bila mimi huwezi kipenzi changu.

 

 

 

Tangia mwanzo nilikujuza mapenzi yangu, nilikufanya uwe wangu wakipekee,

Ulimwengu nalikupa ishara la penzi langu, na vyote nikavitiisha uvimiliki wee,

Roho nikakujaza ushiriki utukufu wangu, chema nilichokuzuia  nikipi niambee,

Ewe tunu ya moyo wangu niambee, nijuze nikijue kipenzi changu.

 

 

 

Japo maliki nilikuumba ukafanywa mtumwa, dhawabu na mamlaka ukayapoteza,

Kakutahadhirisha kwa Neno, ishara, na miujizwa, ila karidhia hila za Mnyang’anyi kikutongoza,

Hukunisadiki hata nilipokuamba atakuuwa, kongwa akakuvisha yakakupata niliokukataza,

Ewe tunu ya moyo wangu nisadiki, nikukomboe kipenzi changu.

 

 

 

Nikasubiri tena kwa saburi sikuoni, mchana kutwa sikuoni usiku kucha uwapi?

Dhalim kakuziba masikio kakupofusha machoni, kakulemaza usinirudie Ewe wangu waridi!

Haki kadai fidia ajili ya wako uhayawani, arbuni kiasi cha bikra kalipa tena kwa hiari,

Ewe tunu ya moyo wangu uwapi, nakudhamini kipenzi changu.

 

 

 

Uhai pia nikatozwa kutosheleza fidia, Utimilifu wa Mungu kautwikisha utumwa!

Aibu, mateso, dhambi hata mauti zote kalipia, dhawabu yako na mamlaka kazitwaa,

Sasa Mimi Ndimi Njia, Kweli, na Uzima, nifuate, nisikize na unitumainie daima,

Ewe tunu ya moyo wangu nifuate, twende zetu nyumbani kipenzi changu.