Monday, 2 June 2014

AGANO JIPYA-(SURA YA 2)



Agano Jipya: Je, kando na Biblia Takatifu kuna ushahidi kuwa Bw. Yesu aliishi?

Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

Fika sasa tumethibitisha dhahiri shahiri kuwa imani kwake Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo kwa mujibu wa Biblia Takatifu ndio halali na njia pekee yetu waja kumjua Mola, Mumba wa vyote. Ithibati hii ndo ili tutamatishia mjadala wetu “Agano Jipya-(sura ya 1).” Leo hii tuking’oa nanga ni vema tujikumbushe angaa kwa kifupi tuliyopitia katika sura ya kwanza, ambapo tuliona jinsi ushahidi ulivyo sheheni dhidi ya matope na matusi inayotupiwa Biblia Takatifu na hususan Agano Jipya. Nashinikiza tena; hakuna chembe wala unywele wa ushahidi unaoweza kusimama dhidi ya Neno imara la Mungu aidha katika asasi yoyote ile au chuo chochote kile cha sayansi au utafiti ulimwenguni mzima.


 

Kwa wengi imani yetu katika Bw. Yesu sio jambo lakutiliwa shaka au kutafutiwa ushahidi. Biblia Takatifu inamnukuu Bwana wa Bwana akituhimiza kuwa imani huja kwa kulisikia Neno la Mungu na wote wanaomjia sharti kwanza waamini Yupo. Zaidi thawabu iliyobora imetengewa wale wamuaminio pasipo kutegemea ushahidi au ishara zinazobainika kwa macho ya mwili. Isitoshe, Wakristo katu hatuna wasiwasi wowote kuwa Masihi, Mtakatifu wa Watakatifu aliiacha enzi ya milele na kuvalia mwili, alitembea hapa duniani na kushiriki maisha kama wanadamu wengine zama zile tunazosoma katika Agano Jipya. Na cha mno, alitimiza yote yaliyotabiriwa na manabii kumhusu.

Ila leo hii Wakristo hatuna budi kujitosa barabara katika ulingo huu wa dhihaka na cheche za matusi ili kuwakomesha na kuwakemea vilivyo mahasidi wote wa imani hii yetu katika Kristo. Lazima tuwajulishe wote wanaofikiri kutushambulia lazima wawe tayari kwa makabiliano ya ana kwa ana bila kutetereka. Mwenyezi, amiri wa majeshi yote ya bingu atutangulie. Amin.

Kama tujuavyo ni ukweli tu ndo utatuweka huru! Kwa wenzetu waliopotoka na wale walio changanywa kwa mafunzo duni ukweli wa mambo ni, ushahidi kando na Biblia Takatifu upo unaothibitisha kuishi kwa Bw. Yesu; amani na hifadhi ya wote wamwaminio. Zafuata ni baadhi ya simulizi toka nyaraka ambazo ziliandikwa na watu binafsi kwa makusudi tofauti.   


Tacitus (C.E. 54-119) 

Alikuwa mwanahistiroia na Seneta katika serekali ya Roma. Katika moja wapo ya nyaraka zake anamtaja Bw. Yesu kuwa mwanzilishi wa imani ya Kikristo; dini ambayo kwa wakati ule ilichukiwa na Warumi. Pia anaongeza kuwa alihukumiwa kifo na Gavana Pontius Pilate enzi za umiliki wa Tiberuis. 



 Pliny the Younger, (C.E. 61-115)

 

Alikuwa mwandishi na Gavana wa Bithynia. Katika moja ya nyaraka alizomwandikia kiongozi Trajan, akitaka ushauri wa hatua atakazochukulia Wakristo walioishi katika himaya yake, mashtaka yakiwa ibada zao. Ibada walizozifanya Wakristo zilenda kinyume na itikadi za kuabudu miungu ya warumi. Kwake yeye Wakristo walimtukuza mtu aliyeishi kama mungu. Kuelezea taratibu na desturi za washukiwa hawa aliandika kuwa, niwaadilifu katika maisha yao na wako na imani dhabiti kwake Bw. Yesu, waliyemuabudu kila uchao kwa nyimbo za sifa pamoja na kushiriki Meza ya Bwana. 

  
Flavius Josephus, (C.E. 37-100):

Nilimtaja hapo mbeleni, alikuwa mwanahistoria ambaye alinakili mambo mengi kuhusu enzi zake. Yanayo tuhusu ni habari alizoandika kuhusu kifo cha Yohana Mbatizaji pamoja na Yakobo (James) aliyemtambua kuwa ndugu ya Yesu aliyeitwa Kristo.

 

Ukweli unapowekwa wazi bila mapendeleo, wote wenye hila hupata haki yao- aibu! Kwa ujumla hakuna ushahidi wowote ule unaozidi yale yaliyomo katika Biblia Takatifu. Isitoshe, Neno la Mungu, Mumba wa vyote halihitaji kutetewa kwa vyovyote vile, maana mtu yeyote aliyenauwezo wa kutathmini mambo hujionea wazi utukufu na ukweli uliopo katika Bilblia nzima. Swali ni, kabla ukumbatie upumbavu, je, Biblia Takatifu umeisoma kwa kina?

No comments:

Post a Comment