Sunday, 29 June 2014

NEEMA YA KRISTO YATOSHA


Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.


Wapendwa natumai bado sote twazidi kumkabidhi nyoyo zetu Kristo- mwanzilishi na mkamilishi wa imani yetu, mlinzi wa kweli na ngome thabiti. Katika hali iyo hiyo, tuzidi kuwaombea wenzetu waliofiwa na jamaa zao ili wapate afueni na ukakamavu wa kuwawezesha kuendelea na maisha. Ni kwake Baba wa mbinguni na hakimu wa dunia yote twaomba atufute machozi ya dhiki tunayopitia. Maana bado umwagikaji wa damu isio na hatia yaendelea nchini mwetu! Licha ya hayo yote Mungu asalia kuwa Mungu. Wakristo wenzangu tujipeni nguvu katika Bwana wa majeshi, yeye hulipisha kisasi cha watu wake kadiri ya neno lake. Kitabuni cha Mwanzo twaelezwa jinsi Mungu alivyoweka sheria kuhusu umwagaji wa damu isio na hatia. Katika sheria hii, alijumuisha binadamu pamoja na wanyama wote; yeyote kati yao atakayemwaga damu ya binadamu atalipa kwa damu yake vile vile. 

 

“Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu. Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu.” Mwanzo 9:5-6.  

 

Kwa hivyo wapendwa tusitamauke! Kauli ya Bwana Mungu wetu ii wazi kuhusu dhuluma na ukatili huu ambao wazidi kutujaza sote majonzi na simanzi isiyotamkika. Wasiwasi na kuhangaika pia tutoe nyoyoni zetu; tusikipe kitu chochote nafasi yakuzima tumaini letu kwake Baba wa milele- daima Mkweli na Mwaminifu. Yakini tusipofanya hivyo twajiweka katika hatari kubwa yakusombwa na majuto kiasi cha kutukatilia mbali na ahadi zake Mola wetu! Ahadi ambazo yeye huinuwa mkono wake wa kuume kutuapia na kwa mkono huo huo ulojaa nguvu na uweza mkuu hututimizia. Ingawa dhiki yatulemea na hofu kutuzunguka kama maji mengi, Wakristo tukubukeni hakuna cha kututenganisha na upendo wa Kristo. 

 

 

“Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Warumi 8: 35-39. 

 

La, ziada ni lipi enyi wateule wa Mungu aishiye milele? Mmejisomea wenyewe jinsi Mtume Paulo, anavyotathimini upendo wa Mungu katika Kristo kwa wote wamuaminio ikilinganishwa na yote yaliyopo na yatakayo kuwepo. Je, Mt. Paulo kafikia aje uthabiti huu katika imani yake? Kwa kuwa Muisraeli? Kwa kuwa Muebrania? Kwa kuwa uzao wa Ibrahimu? Nawaulizeni neno hili kwa kuwatakieni mbaki imara katika upendo uo huo wa Kristo Yesu, kisha tuwatie nguvu wale wanyonge miongoni mwetu. Maana majaribu yanapotupata upendo wetu kwake waweza anza kufifia halafu kuwa baridi sawasawa na mbegu iliyoanguka kwenye mwamba (Lk. 8:13). Walakini, imani iliyoimarika mithili mlima wa jabali kama yake Mt. Paulo, hupatikanaje? 

 

 


Katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. Kwa wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja. Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini; katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyanganyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi.”  2Wakorintho 11:23(b)-30

Haya basi wapendwa, kilio kisituzidi, dhiki isituzamishe wala majuto kutufarakanisha na Bwana wetu atupendaye zaidi ya uhai. Tuzikazeni nyoyo zetu kumtumainia, na kutakasa njia zetu ili azidi kutufadhili, aidha hata nao watesi wetu tuwaombee Mola wetu akapate kuwaonekania kwa wingi wa kudura zake. Kwa namna hii, wote watakaoona hivi watapata kustaajabu na kurudi nyuma! Ila kwetu sisi ndugu wapendwa tuzidisheni kuikumbatia bila kuachilia thawabu hii tuliyopewa na Kristo, yaani neema toka kwake Mungu wa kweli. Natuilindeni zaidi ya vyote tulivyo navyo hata uhai wetu, maana, “mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza na mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona” (Mat.10:39). Ni kwa azma hii pekee ndipo nasi pia tutaweza kujibu kwa ujasiri kama Shadraka, Meshaki na Abednego walipo hukumiwa kifo kwa kutosaliti imani yao…..

 

 

“Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.” Dan. 3:17-18.


Na atukuzwe Mungu Baba yetu, Mungu pekee mwenye enzi ya milele na milele na Bw. Yesu Kristo utimilifu wake ulimwenguni kote. Amin.

 

No comments:

Post a Comment