Sunday, 8 June 2014

JUKUMU LILOJAA BARAKA TELE TELE


 



Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.


Kama nilivyotarajia hawa “wasomi” hawana lolote la msingi kutueleza. Unapowakabili kwa shahidi zilizopo wala sio majibizano bila mwisho kama ilivyo hulka yao wananyamaa utadhani wamesadiki ukweli wa mambo. Lakini kama mababa zao waliokaidi amri za Mungu na kuwaua mashahidi na manabii wa Bwana wa majeshi ndivyo walivyo hata leo hii. Wote huja kwa maneno matamu na tungo za kila aina za kuzua ubishani ilikujionesha wenye hekima na walioacha “ushamba” na “kuendelea mbele.”

 

“Maskani zako zapendeza kama nini, Ee Bwana wa majeshi! Nafsi yangu imezionea shauku nyua za Bwana, Naam, na kuzikondea. Moyo wangu na mwili wangu Vinamlilia Mungu aliye hai.”  Zaburi 84: 1-2

 

Enyi aila yake Mtakatifu wa Watakatifu, Mungu wa Kweli na Aishie milele aliyetufanyia wokovu kupitia Mwanawe wakipekee ambaye ndiye Utimilifu wa Mungu katika mwili-Bw. Yesu Kristo, msidanganyike! Wengine kati yetu watauliza mbona anatoa tahadhari hii na wengine kusema anatutisha bure. La! Hasha, wateule wa Bwana. Kusudi langu nikuupoza ukulele wa shangwe ambao umeanza sikika miongoni mwetu; ati shangwe? Enhee, shangwe! Maana kuna wale tayari washaanza kusherehekea kimya cha mahasidi wetu. Wanachukulia huko kutoweza kwao kujibu hoja zilizotangulia kuwa ni ushindi.

 


Ila adui haanguki aliporushwa na utulivu huja kabla ya dhoruba kali. Misemo hii nakuabieni ili msilegee katika dua zenu wala kuzama katika Maandiko Matakatifu. Maana Asipoenda nasi yote ni ubatili. Kama Nabii Musa alivyotambua karne nyingi zilizopita ushindi haupatikani kwa ncha ya upanga au kwa wingi wa makombora wala kwa ushupavu na wingi wa majeshi, bali kwa uwepo wa Mungu Baba peke yake. Hapa najua wapumbavu watadhihaki na wale jeuri kati yao watatusi na kutema mate chini. Kwenu nitawakumbusheni sio mara moja majeshi yaliyojizatiti kwa silaha na makombora mazito mazito kushindwa na wanyonge: Katika vita vya kupigania Uhuru wa Kenya nani alicharaza majeshi ya Malkia wa Uingereza? Na, je, taji la ushindi halikutwaliwa na akina yakhe waliokuwa washamba kupindukia; watoto wa wakulima, wafugaji, wavuvi na walalahoi! 

 


Mungu wa kweli; ambaye amejitambulisha ulimwenguni mzima kitimilifu katika Bw. Yesu Kristo, daima huwatetea wanyonge na kuwaaibisha wenye kiburi. Basi, tusikae kitako na kungoja hadi adui watakapojikusanya upya na kutushambulia ghafla! Hata bila majibu toka kwao, tusikome kumcha Mungu wetu wala kulishangilia Jina lake lenye Uwezo na Neno lake kulieneza kote kote pasina kuchoka au kususia jukumu hili lilojaa baraka tele tele, tena za kila aina. 





Kwenu Wakristo wenzangu, mboni la jicho lake Mwenyezi, tusiwedhaifu bali tuweniwaadilifu. Tuukazeni mwendo Mkombozi wetu akitutangulia. Na kwa wale kati yetu wamerudi nyuma, Mungu Baba ni mpole wa hasira lakini mwepesi wa fadhila rudi nyumbani ewe mpendwa kwa hakika atakulaki kwa rehema, la ziada nikuwa faraja yako baado ipo mkononi mwake. Isitoshe, kazi baado nyingi nyumbani mwa Baba hutakosa la kufanya ili kuchangia kurejea kwake Mfalme wa Wafalme.

No comments:

Post a Comment