Neema
na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

Nimetatizika
sana jinsi nitakavyo anza kukuelezeni kuhusu mada ya leo. Uzito nilionao moyoni unanifanya nishindwe kujieleza vizuri, sawa-sawa nawe Mkristo Mwenza na Mzalendo
mwenzangu, pamoja twaililia nchi yetu kwa uchungu usioelezeka. Hali hii ya mshikemshike imetufika
sisi sote bila kubagua kabila, cheo, dini, au umri. Wakristo hapa nawakumbusheni
kuwa mmoja wetu akiguswa sote tumeguswa, mmoja wetu akiadhirika sote
tumeadhirika. Kabla ya kuendeleza mengine: Pole zangu za dhati ziwafikie wote walio
wapoteza jamaa na familia. Hakuna kinachoweza kuchukuwa nafasi ya wapendwa wetu
waliotuacha ghafla tena kwa njia ya kikatili mikononi mwa magaidi. Mwenyezi awape nguvu katika kipindi hiki kigumu. Amin.
Vile vile
wapendwa nigependa tukumbuke kuwa ingawa ni vigumu kukubali yaliyotendeka sasa ndo wakati wa kuvalia imani yetu barabara na kwa ujasiri. Musinielewe visivyo;
tumeona walengwa wa mashambulizi haya ni akina nani na maswali wanayoulizwa
ndugu zetu kabla kupewa hukumu ya kifo. Wanaotutenda haya wanabagua waziwazi
kati ya nani watamwacha hai na nani watampokonya uhai wake. Msingi wa matendo yao wameweka wazi; hapa hakuna cha ati ati, na sio
mwengine bali ule ule wakudhalalisha imani yetu katika Kristo, nakutaka kufanya
imani katika Masihi wa Mungu kama si kitu! Ila ewe uliye katikati moyoni mwa Mungu
wa Kweli usifadhaike wala kuaibika. Bado Mungu wetu yuko pamoja nasi.
Wapendwa, nitawahimiza tena;
tusione yale tunayopitia kama mageni, la, njia hii ni ile iliyonyooka mpaka
kifuani mwake Bw. Yesu. Hapa nitawakumbusheni ndugu zetu wawili walio
tutangulia: Mkubukeni ndugu yetu Stefano, alivyokazania imani katika Kristo,
alivyozidi kuhubiri Ufalme wa Mungu hata wakaanza kumpiga kwa mawe na Mbingu
zikafunguka. Kipigo alichokuwa akipokea hakikumzidi kwa lolote maana Roho wa Utukufu na wa Mungu alimjaa. Badala yake kulia kwa uchungu aliwalilia watesi
wake wasamehewe!
Mkumbukeni Yohana, aliyefunuliwa
siku ya Kiama ya kurejea kwake Bw. Yesu kwa ushindi pamoja na maelfu ya maelfu
mia elfu ya Wateule wake kuhukumu Ulimwengu. Kabla yakupofushwa kwa kutolewa
macho kwa kutumia upanga uliotiwa moto watesi wake walimtosa katika debe kubwa la
mafuta yanayotokota na hakupoteza hata uzi wa pindo la vazi lake. Walipoona wameshindwa kumuua ndipo walimtupa kisiwa cha Patmos, katika hali hiyo ya upofu na majeraha mengi aliyokuwa nayo ndipo Bw. Yesu akamtokezea na kumfunulia kitabu tunacho kienzi; Ufunuo wa Yohana (Revelation). Je, Mpendwa utasema hawa walitelekezwa au kuachwa na Mchungaji wao Mwema? Sisemi Enoko, Elijah, Musa, Ayubu, Yakobo, Samsoni ............... hatuwezi wataja wote hadi leo hii, wewe na mimi tukiwepo mle ndani pamoja na hawa ndugu zetu waliotangulia mbele zetu, maana tunaabudu Mungu yule yule habadiliki milele na milele. Amin.
Basi
tutasema nini Wapendwa; Mungu Baba ametuacha, ametupeana tuangamizwe na
kuaibishwa hadharani, la, hasha! Kwa mujibu wa Neno lake Takatifu na Tukufu, mateso na
misiba hutufika sisi kwa maksudi yake Mungu Baba yetu. Sijakosea Mpendwa. Nitarudia tena ili tufahamiane vema, mateso na
misiba hutufika sisi kwa maksudi yake Mungu Baba yetu. Maana Anasema kwa yule nimpendaye lazima nitamrudi, sababu ikiwa, katika mateso hapo
ndipo sisi hufanywa watimilifu katika imani yetu. Kwa hiyo waona Mpendwa kusudi lake
Mungu wetu halijabatilishwa wala kubadilika juu ya maisha yako au yangu, asha! Kusudi
lake nituwe imara tena dhabiti katika imani ilituweze kushinda yote ya dunia
hii ambayo mwisho wake imeandikiwa adhabu kwa uovu na damu
iliyomwagwa ndani yake isiyo na hatia toka Habili (Abel). Bali kwetu sisi aila yake Mwenyezi, maana Bw. Yesu Mwenyewe
atuita ndugu zake, sisi tumeandikiwa urithi wa uzima milele. Hakuna cha kututenganisha na upendo wa Kristo. Basi tunapoliwaza ndugu zetu na kuzidi katika shughuli za kila siku, tukumbukeni yote ni kwa Jina lake Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Amin.
No comments:
Post a Comment