Neema na iwe kwenu na amani,
zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
Wapendwa natumai bado sote twazidi kumkabidhi nyoyo zetu Kristo-
mwanzilishi na mkamilishi wa imani yetu, mlinzi wa kweli na ngome thabiti. Katika
hali iyo hiyo, tuzidi kuwaombea wenzetu waliofiwa na jamaa zao ili wapate
afueni na ukakamavu wa kuwawezesha kuendelea na maisha. Ni kwake Baba wa
mbinguni na hakimu wa dunia yote twaomba atufute machozi ya dhiki tunayopitia.
Maana bado umwagikaji wa damu isio na hatia yaendelea nchini mwetu! Licha ya
hayo yote Mungu asalia kuwa Mungu. Wakristo wenzangu tujipeni nguvu katika
Bwana wa majeshi, yeye hulipisha kisasi cha watu wake kadiri ya neno lake.
Kitabuni cha Mwanzo twaelezwa jinsi Mungu alivyoweka sheria kuhusu umwagaji wa
damu isio na hatia. Katika sheria hii, alijumuisha binadamu pamoja na wanyama
wote; yeyote kati yao atakayemwaga damu ya binadamu atalipa kwa damu yake vile
vile.
“Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama
nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai
wa mwanadamu. Atakayemwaga
damu ya mwanadamu,
damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu.” Mwanzo 9:5-6.
Kwa
hivyo wapendwa tusitamauke! Kauli ya Bwana Mungu wetu ii wazi kuhusu dhuluma na
ukatili huu ambao wazidi kutujaza sote majonzi na simanzi isiyotamkika.
Wasiwasi na kuhangaika pia tutoe nyoyoni zetu; tusikipe kitu chochote nafasi
yakuzima tumaini letu kwake Baba wa milele- daima Mkweli na Mwaminifu. Yakini
tusipofanya hivyo twajiweka katika hatari kubwa yakusombwa na majuto kiasi cha
kutukatilia mbali na ahadi zake Mola wetu! Ahadi ambazo yeye huinuwa mkono wake
wa kuume kutuapia na kwa mkono huo huo ulojaa nguvu na uweza mkuu hututimizia.
Ingawa dhiki yatulemea na hofu kutuzunguka kama maji mengi, Wakristo tukubukeni
hakuna cha kututenganisha na upendo wa Kristo.
“Ni nani atakayetutenga na upendo wa
Kristo?
Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama
ilivyoandikwa, ya kwamba, kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, tumehesabiwa
kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda kwa yeye
aliyetupenda.
Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala
malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye
uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote
hakitaweza kututenga
na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Warumi 8: 35-39.
La,
ziada ni lipi enyi wateule wa Mungu aishiye milele? Mmejisomea wenyewe jinsi
Mtume Paulo, anavyotathimini upendo wa Mungu katika Kristo kwa wote wamuaminio
ikilinganishwa na yote yaliyopo na yatakayo kuwepo. Je, Mt. Paulo kafikia aje
uthabiti huu katika imani yake? Kwa kuwa Muisraeli? Kwa kuwa Muebrania? Kwa
kuwa uzao wa Ibrahimu? Nawaulizeni neno hili kwa kuwatakieni mbaki imara katika
upendo uo huo wa Kristo Yesu, kisha tuwatie nguvu wale wanyonge miongoni mwetu.
Maana majaribu yanapotupata upendo wetu kwake waweza anza kufifia halafu kuwa
baridi sawasawa na mbegu iliyoanguka kwenye mwamba (Lk. 8:13). Walakini, imani
iliyoimarika mithili mlima wa jabali kama yake Mt. Paulo, hupatikanaje?
“Katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika
mapigo kupita kiasi; katika
mauti mara nyingi.
Kwa wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja. Mara tatu
nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa
jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini; katika kusafiri mara nyingi;
hatari za mito; hatari
za wanyanganyi; hatari kwa taifa langu;
hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za
baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika
taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi.” 2Wakorintho 11:23(b)-30
Haya
basi wapendwa, kilio kisituzidi, dhiki isituzamishe wala majuto kutufarakanisha
na Bwana wetu atupendaye zaidi ya uhai. Tuzikazeni nyoyo zetu kumtumainia, na
kutakasa njia zetu ili azidi kutufadhili, aidha hata nao watesi wetu tuwaombee
Mola wetu akapate kuwaonekania kwa wingi wa kudura zake. Kwa namna hii, wote watakaoona
hivi watapata kustaajabu na kurudi nyuma! Ila kwetu sisi ndugu wapendwa tuzidisheni
kuikumbatia bila kuachilia thawabu hii tuliyopewa na Kristo, yaani neema toka
kwake Mungu wa kweli. Natuilindeni zaidi ya vyote tulivyo navyo hata uhai wetu,
maana, “mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza na mwenye kuipoteza nafsi yake kwa
ajili yangu ataiona” (Mat.10:39). Ni kwa azma hii pekee ndipo nasi pia tutaweza
kujibu kwa ujasiri kama Shadraka, Meshaki na Abednego walipo hukumiwa kifo kwa
kutosaliti imani yao…..
“Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye
atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali
kama si hivyo,
ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi
hatukubali kuitumikia miungu yako,
wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.” Dan. 3:17-18.
Na
atukuzwe Mungu Baba yetu, Mungu pekee mwenye enzi ya milele na milele na Bw. Yesu Kristo utimilifu wake ulimwenguni kote. Amin.