Monday, 29 September 2014
Monday, 22 September 2014
HAMMO GIZANI: MMEKUWA WANA WA NURU NA WANA WA MCHANA (SURA YA 3)
Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
Mungu Baba, Ewe, Muumba na Muumbuaji, twakuabudu na kunyenyekea mbele zako kwa ajili ya ukuu na uweza wako maishani mwetu. Tukikushukuru kwa yote unayotutendea, Ewe, usiye na hila wala uovu ndani yako, Baba mwema, unayetufahamisha makusudi yako kabla huja tenda jambo lolote. Daima mkweli na daima mwaminifu, Jalali, tuzidishie uwepo wako siku kwa siku ili tuweze kuukabili ulimwengu na maovu yake yote na zaidi tukaweze kukujua vema na kutembea nawe kwa imani hadidi tukiufuata uelekezi wako, Ewe, mchungaji mwema wa maisha yetu. Amin.
Wapenzi wa Mungu, enyi manukato yake Kristo Yesu, utimilifu wake Mungu Baba nawasabahi na kuwakaribisha katika somo la leo. Shabaha letu likiwa lile lile, kuzidi kujifunza Neno Takatifu la Mungu Baba yetu. Kama ilivyo desturi yetu, kwanza tutajikumbusha kwa kifupi yale tuliyosoma wiki jana; tulisoma kuhusu aliyekuwa Mfalme wa Yuda kwa jina Yosiah, na jinsi alivyotumika na Mungu kuwarejesha watu wake katika imani na ibada ya kweli. Kadhalika tuliona jinsi Mungu Baba alivyoahidi kumimina Roho wake kwa wote wenye mwili katika nyakati hizi za mwisho na kuwa atamuinua mtu atakaye tumika kama Mfalme Yosia alivyotumika, ili awatayarishe watakatifu wa Mungu wakaweze kumpokea Roho Mtakatifu atakapomiminwa. Jambo la msingi likiwa kuwawezesha watakatifu kujihami kiroho na kuimarika kiimani ili wakaweze kustahimili wakati mgumu utakaoifika dunia nzima sawa na Neno la Mungu wa Israeli alilozungumza kupitia vinywa vya manabii wake.
Somo la leo la ng’oa nanga kwa kuufuata mkondo ule tulioushika wiki jana na kuendelea kuchunguza umuhimu wa Roho Mtakatifu kumiminwa juu ya wote wenye mwili katika siku hizi za mwisho. Mwongozo wetu tunautoa toka mfano ule wa wanawali kumi, (MAT. 25: 1-13). Lakini, kabla ya kuuchambua mfano huu ni vema tuelewe kiini chake, yaani mbona Bw. Yesu akafunza vile na kusudi lake lilikuwa lipi kwa wasikilizaji wake. Ukirudi nyuma kidogo aya ya 24, hapo ndipo funzo nzima la anzia. Bw. Yesu atoka hekaluni na kuukwea mlima wa mizeituni ili apumzike, huku wanafunzi wake wakimwonyesha utukufu na ustadi wa Hekalu. Bali Bw. Yesu akawazungumzia na kubashiri yatakayojiri kwa muda usio mrefu, nao wakamwendea kwa faragha na kumuuliza awaeleze lini mambo hayo yote yatatendeka na nini dalili ya kuja kwake na ya mwisho wa dunia. Jibu alilowapa na maelezo yake yakajumuisha matukio mbali mbali yatakayo tendeka duniani kote katika nyakati za mwisho na akazidisha hata kuwanenea kwa mifano; mfano huu wa wanawali kumi na hata ule unaoufuata wa talanta ni katika jumla ya maelezo yake Kristo Yesu. Hata hivyo hatutashughulika na mfano huo wa talanta kwa sasa, lakini ifahamike kuwa sijamzuia mtu ye yote kujizulia baraka toka mfano huo, kwani Neno la Mungu liwazi kwetu sote.
Bila pingamizi, mfano huu wa wanawali kumi, q Bw. Yesu aliunena ukiwa mojawapo kati ya maelezo yake alipolijibu lile swali aliloulizwa na wanafunzi wake kuhusu, nini dalili ya kuja kwake na ya mwisho wa dunia. Kwa mukhutasari, katika mfano huu wa wanawali kumi, anaufananisha Ufalme wa mbinguni na sherehe ya harusi ambayo ikishaandaliwa bwana harusi akakawia kufika mpaka giza likaingia akiwa baado hajafika na hata waliokuwa wamejiweka tayari kumlaki wakalala. Cha muhimu ni kuwa sherehe haikuvunjwa na ijapokuwa bwana harusi alichelewa hatimaye aliwasili kukiwa usiku wa manane na kulakiwa na baadhi ya waliostahili kumlaki. Sababu ikiwa sio wote waliokuja harusini walikuwa wamejitayarisha vilivyo kwa sherehe, ilhali kwa kuzibeba taa zao yaonekana wote walikusudia kuwa bwana harusi angekawia kufika na hata kuchelewa hadi usiku umpate angali hajafika.
Fika hapa, nadhani ni wazi kwetu sote kuwa Bw. Yesu anaelezea mambo yaliyo nyeti sana tena kwa mafumbo, dhamira yake ikiwa ni kuwafunulia mambo yaliyositirika katika Roho wa Mungu kwa njia watakayoelewa kwa urahisi. Hivi ni kumaanisha kwamba, jibu alilowapa wandani wake na maelezo yale yaliwahusu moja kwa moja, kwani toka kwao Kanisa (Mwili wa Kristo), lilipata mafundisho yake Kristo; ambayo ndiyo msingi wa ibada, itikadi na kanuni za Ukristo. Msingi wa imani ya Ukristo ni kuwa tumaini tulionayo katika ukombozi wake Kristo Yesu utatimilika atakaporudi kuwachukuwa wote waliowake toka duniani na kuwapeleka mbinguni halafu ataihukumu dunia. Pasi na tumaini hii kuwepo katika imani ya Mkristo, bila shaka imani ile imepungukiwa, kwa kuwa imepuuza ushahidi mzima wa kufa na kufufuka kwake Mkombozi wetu Yesu Kristo. Maana, katika kifo na kufufuka kwake Mkombozi wetu alitimiza kazi yake ya kuukomboa ulimwengu na kuupatanisha na Mungu Baba na baada ya kufufuka alijidhihirisha kwa wanafunzi wake kisha akapaa juu mbinguni kwa ahadi kuwa atarudi tena (kama mwizi) kuwachukuwa wote waliowake ili wawe pamoja naye mahali alipo.
Mfano huu wa wanawali kumi, haswa, unaelezea ujio huu wa Bw. Yesu kama mwizi na jinsi watakatifu wake wanavyostahili kumsubiri yeye bwana harusi wakiwa wamejiandaa vilivyo, kwa kuwa ameandaa sherehe na hataghairi bali atakuja, hata kama atachelewa na kufika usiku katikati kwenye giza kuu lazima atakuja. Fika hapa ningependa tutilie maanani wanawali wale kumi. Tayari tumeona wanaashiria watakatifu wote wamwaminio KristoYesu, yaani, Kanisa, na ndio maana tunajulishwa kuhusu unawali/ubikra wao. Kwa hiyo hakuna sababu maalum yakutofautisha kati ya wale tano wenye busara na wale tano wapumbavu kwa msingi kuwa wale tano wa kwanza ndio wanaoashiria Kanisa ilhali wenzao wanaashiria walimwengu (watu wasio na imani katika Kristo Yesu). Hebu tutazame vema maelezo tunayopewa kuwahusu.
Wote kumi ni wanawali/mabikra
Wote kumi walialikwa sherehe kumlaki bwana harusi
Wote kumi walitwaa taa zao ila tano kati yao ndio walio twaa pamoja na mafuta katika vyombo vyao
Tokana na maelezo haya tunaona kuwa wote walikuwa watakatifu bila unajisi wo wote; ubikra,(2KOR. 11:2). Tena wote walikuwa wamealikwa katika sharehe ile kumlaki bwana harusi, hii ina maana kuwa walikuwa na ufahamu wa harusi ile na zaidi walikuwa maswahibu ama ukipenda wandani wake bwana harusi kwa lile jukumu waliloteuliwa kutimiza, yaani, kumlaki atakapowasili. Isitoshe wote walitwaa taa zao, kuonyesha walikusudia kuwa bwana harusi angelichelewa kwa kuwa hakuna aliyetamauka na kwenda, bali walimngoja hadi usiku wa manane, hii ina ashiria imani yao. Sawa na hayo, taa kama tujuavyo huashiria Neno Takatifu la Mungu, (ZAB.119:105) na mafuta huashiria Roho Mtakatifu, (KUT. 29:7; 1SAM. 16:13). Kama wote ni watakatifu na wateule zake bwana tena wenye imani kwake na wanalishika neno lake (taa), basi mbona baadhi yao (wale tano wapumbavu) hawakuruhusiwa kuingia harusini licha ya bidii yao na kujitolea kwao?
Wapendwa kama tulivyoona wote kumi walikuwa hali sawa isipokuwa kwa mafuta. Kama nikujitenga na ulimwengu na yote yanayoweza tia utakatifu wao najisi wote walifaulu. Kama ni kuwa na imani kuwa bwana harusi atakuja wote waliamini. Tushikilie hapo kwanza, na kutazama kuwa wote ilifika pahali wakasinzia na kulala, maanake ni, imani ya kuwa bwana harusi atakuja ili didimia sawa na kukawia kwake kulivyo zidi; kukawia kule kunaashiria majaribu. Ila bwana harusi alipowasil na wote wakatoka nje kwenda kumlaki kuna wale kati yao hawakutwaa mafuta pamoja na taa zao kwa hiyo taa zao hazikuwaka. Kuzimika kwa taa zile kwa kukosa mafuta kunaashiria kupoteza imani na Neno la Mungu na badala yake kutegemea matendo makavu pekee. Vile vile, kutokuwa na mafuta kunaashiria kutopokea ubatizo wa Roho Mtakatifu. Na huku kukosa mafuta ndio sababu ya taa zao kuzima na kutoweza kuwaka tena, hali kadhalika ikiwa ndiyo sababu yao kufungiwa nje na kutokubaliwa kuingia katika sherehe pamoja na bwana harusi. Kumbuka ilimfaa kila mmoja awe na mafuta chomboni mwake. Naye bwana harusi siye mwingine ila ni BWANA YESU KRISTO, (YN. 3:26-29).
Naye ndiye anayetueleza kupitia mfano huu kuhusu kuja kwake, ili tujiweke tayari kwa kutimiza yote yanayohusu imani na utakatifu. Na tunapofanya hivi isiwe kwa akili zetu tu na vile tunavyodhania mambo yatatukia, bali tumtegemee Roho Mtakatifu kutuangazia Neno lake hadi mwisho ili taa la tumaini letu lisizimike kwa kukosa mafuta wakati giza na majaribu yatakapozidi na Bwana wetu aonekane kukawia kuja, (YN. 16:13-15). Fika hapa, tunaona wazi kuna baadhi ya Wakristo watakaoachwa nyuma na Bwana atakapowakujia waliowake, (MAT. 7:21). Bali wapendwa isiwe hivyo kwetu sisi, nafasi baado tunayo hivi sasa kubadili mienendo yetu na hususan mtazamo wetu kuhusu Neno Takatifu; tuitisheni Roho Mtakatifu, na kutegemea uweza wake ili atuimarishe katika imani kwa kutuongoza katika kweli yote na kutupasha mambo yatakayotendeka hadi atapokuja BWANA YESU KRISTO kutuchukua. Na atakapokuja sisi tutamlaki kwa furaha, shangwe na nderemo maana atatupata tukiwa watimilifu kumpokea na bila shaka atatukubalia kuingia pamoja naye mbinguni alikotuandalia sherehe, (UFU. 19:9).
Sijazungumzia wanaouza mafuta, hawa ni makuhani/watumishi wa Mungu (ISA. 24:1-3; MAT. 7:21-23)
Sunday, 14 September 2014
HAMMO GIZANI: MMEKUWA WANA WA NURU NA WANA WA MCHANA (SURA YA 2)
Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
Mungu mwenye enzi ya milele na milele, tunakutukuza na kukushukuru kwa wema na rehema zako maishani mwetu. Maana, Ewe ndiwe Muumba wa vyote, iwe ni juu Mbinguni, hapa Duniani na Ulimwenguni mzima. Vyote vinavyoonekana na visivyoonekana viko chini ya uweza wako kwa kuwa vyote vinakuhitaji na kukutegemea Ewe, Mungu, Muumba na Muumbuaji. Isitoshe, hakuna kinacho weza kufananishwa nawe, kwa kuwa hauhitaji chotote au kumtegemea ye yote. Hauna mwanzo wala mwisho bali mwanzo na mwisho ni kazi yako Ewe, Alfa na Omega. Daima uhimidiwe na utukuzwe. Amin.
Tumejaliwa wiki nyingine na Bwana wetu, kwa hiyo tusilegee katika ibada na kumtumikia kwa mali zetu zote na katika kila hali, maana vyote tulivyo navyo ni vyake Yeye Karima, (RUM. 11:33-36). Kwanza tutarejelea somo la wiki jana kimukhtasari; tuwezaona umuhimu wa maombi na kusoma Biblia Takatifu kwa maisha ya mwanadamu na zaidi kwetu sisi Wakristo. Vile vile kuhakikisha kuwa kwa njia hii watakatifu wa kale walipata kujua mawazo ya Mola, na kuwezeshwa kutenda yaliyo sawa na mapenzi yake katika zamani zao. Sawa sawa na hayo tulitambua kwamba, hakuna njia mbadala kwetu sisi watakatifu wa zamani hizi ikiwa twataka kutenda mapenzi ya Mola wetu na kuhesabiwa haki mbele zake, (2TIM. 2:14-15; SEF. 2:3). Basi, enyi wapendwa katika Kristo Yesu, tuzidi jibidiisha katika njia hii tukiwakumbuka watakatifu wote aidha wawe wa madhehebu yetu au la, kwani sote tu viungo vya mwili mmoja (Kanisa) ambaye kichwa chake ni Kristo Yesu, (KOL. 1:13-18; 1KOR. 1:10-13).
Nasisitiza hivi kwa kuwa muda uliopo ni mfupi mno; saa ya kuja kwake Bw. Yesu kulichukua Kanisa lake imewadia! Walakini, Mkombozi wetu hatakuja bila kutuarifu na kutufanya tuwe tayari kwa ujio wake, sawa na enzi za kale Mungu alipotaka kutenda jambo kwanza aliwafahamisha watu wake. Aliwainua manabii kati yao na kuwapa karama na vipawa vya kila aina ili kuwafunza na kuwahubiria watu; wanyoshe njia zao na kuacha dhambi. Wajiweke tayari kwa ujio wa Mungu, aidha kwa rehema au hukumu. Mimi na wewe mpendwa hili ndilo jukumu letu katika kizazi hiki, tujitakase ili tupate kukubalika mbele za Mungu kwa maneno yetu pamoja na mwenendo wetu tuwafae wengi kwa kuwakumbusha utakatifu na utukufu wa Mungu. Wengi wakapate kuutazama mfano wetu na kumrudia Mungu Baba na kujengeka katika imani, huku tukiitazamia SIKU YA BWANA, (YOE. 2:17; 1PET. 2:9-10).
Wapendwa, msichukulie ni tashtiti wala kuchoshwa nakuhimiza kwangu; si ati sifahamu kuwa mambo haya ni ya msingi katika jumuiya nzima ya Wakristo, ila nawapeni tahadhari ya kwamba kila nabii aliyeitabiri SIKU YA BWANA alishinikiza kuwa yaja upesi! Sasa itakuwaje kwetu sisi ambao dalili zote zaonyesha kuwa enzi hii tuishio ndiyo waliotabiri kuihusu? Inatulazimu sote tunaompenda Kristo Yesu kwa nia moja tushirikiane kuimarisha mwili wa Kristo ko kote tuliko; nyumbani, shuleni, hata kazini, (2KOR. 5:1-10). Hasa, yatupasa kutambua yale Mungu Baba ameyaweka tayari kwa ajili ya watu wake katika kipindi hiki, ili tujihami vilivyo na yatakayo ikuta dunia hii hivi karibuni kama tulivyoona katika masomo yaliyotangulia. Pia katika hayo tuliyosoma tulitambua zama hizi za leo za fanana zamani zile za Ufalme wa Yuda, kabla Mfalme Nebukadneza kuuvamia na kuupiga Ufalme ule kwa upanga. Na jinsi Mungu alivyofanya juu chini kupitia manabii wake ili awanusuru watu wake lakini wao walizidi kumkaidi hadi hukumu yake Mungu ilipowafikia sawa na yale aliyoyanena kwa vinywa vya manabii wake.
Kipindi hicho cha Ufalme wa Yuda kilichofanana na enzi hii yetu kilianza na umiliki wa Mfalme Manase. Mfalme huyu, aliijaza Nchi ya Yuda damu isiyo na hatia na kuwapotosha watu wa Mungu kwa kutenda kila aina ya maouvu mpaka kuleta sanamu hekaluni na kumtoa mwanawe kafara kwa hiyo sanamu papo hapo hekaluni!....... Eeh, sitayarudia yote tuliyozungumzia, ila nataka kuwakumbusheni katika kipindi hicho kuna Mfalme mmoja aliye tenda tofauti na matendo ya wenzake, enhe, si mwingine ni Mfalme Yosia. Yeye ndiye aliye haribu sanamu hizo za Mfalme Manase, na kutoa amri Hekalu likarabatiwe na ibada pamoja na matoleo ya kila siku ya rejeshwe kama hapo awali. Kupitia juhudi zake Yuda ikapata muamko mkuu wa imani na kumrudia Mungu wa Israeli. Kwa kifupi nasema hivi, sawa na vile tulivyoona enzi hiyo ya kale ikiwa kioo cha enzi hii ya leo, hivyo ndivyo twatarajia kutatendeka, (2FAL. 22-23).
Mungu atamwinua mtu atakaye tumika kuleta uamusho katika Kanisa lake kabla hajatekeleza hukumu yake duniani. Tofauti itakayokuwepo ni kuwa sote tutakaokuwa tumesafisha “nguo zetu” na kuwa safi tutashiriki katika uamusho huo. Uamusho huu ndio utatimiza kwa utimilifu neno lile alilolinena Nabii Yoeli kuhusu Roho wa Mungu kumiminwa juu ya wote wenye mwili kabla ya SIKU YA BWANA, (YOE. 2:28-32). Kanisa tujiwekeni tayari, Mungu anakusudia kutenda mambo makuu katika Mwili wa Kristo na kisha autumie kwa uweza na utukufu kuhubiri Ufalme wake kabla haja ihukumu dunia hii kwa moto.
Sunday, 7 September 2014
HAMMO GIZANI: MMEKUWA WANA WA NURU NA WANA WA MCHANA (SURA YA 1)
Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
Wapenzi na ndugu katika Kristo Yesu, tuliinue jina lake Muumba wa vyote kwa wingi wa karama zake maishani mwetu, hususan, sisi aliyotuzaa kwa asili ya Roho na moto. Kwa Roho Mtakatifu ametufanya upya; watu wasioongozwa na tamaa za mwili ambazo huishia mauti, bali watu wanaoongozwa kwa nia ya Roho ambayo huishia uzimani. Ametufanyia na amani katika Kristo Yesu, utimilifu wake Mwenyezi, Mungu Baba, asiyeonekana kwa macho. Tuzidishie Ewe, BWANA wetu wema na rehema zako ili tuijue na kuishika njia yako kwa uhakika, tukikutazamia kufunuliwa kwako. Amin.
Watakatifu kwa Neema ya Kristo Yesu, hadi sasa sidhani kama kuna ye yote ambaye tumeacha nyuma kuhusiana na mchakato mzima wa ‘Vipindi Saba Vya Neno La Mungu.’ Tumejadili mambo kadha wa kadha chini ya kichwa hiki kwa muda unaozidi majuma manne hadi sasa. Utaratibu huo umetuwezesha kuweka msingi thabiti wakutuwezesha kusoma na kuelewa chuo cha Ufunuo wa Yohana. Kitabu ambacho kinaogopwa na wengi nakutazamwa kama fumbo kubwa lisiloweza kufumbuliwa, hivi kwamba wengi wetu hatushughuliki kukisoma kabisa!
Muda wake umetimia, kwa kuwa yaliyoandikwa kwa mafumbo enzi za kale Bwana ameyaweka wazi zamani hizi. Hebu nikuulizeni, enyi wateule zake Mungu Baba, ni Neno lipi, hata moja litokalo kinywani mwa Baba lafaa kukupita? kama jibu ni hakuna hata moja. Basi tujibidiisheni kukisoma, maana, aliyotaka tuyajue ameyaweka wazi, na zaidi anatuhimiza kulijua na kulitenda Neno lake. Sadfa na hayo, katika utangulizi wa chuo cha Ufunuo wa Yohana, baraka spesheli imeahidiwa ye yote awaye Yule atakaye soma na kuyashika yaliyoandikwa humo, (UFU. 1:3).
Nafanya kurudia: fika hapa tumekuwa tukiangazia historia nzima ya ulimwengu tangu mwanzo hadi mwisho; Siku ya Kwanza hadi Siku ya Saba. Kati ya siku hizi, Siku ya Tano ndiyo tuliyoishughulikia kwa kina, maana, tulitambua siku hii ndiyo tuiishio kwa wakati huu. Kwa hiyo hatuna budi kuifahamu ili tusiishi sawa na watu wa mataifa pasi na kutathimini yanayotukia kila uchao au baadaye matokeo yatakuwa ya namna gani. Kama wenye hekima ya kweli kati ya wanadamu inatupasa zaidi sisi Wakristo kuwa macho na kufahamu vema zamani hizi tuiishio. Tukizingatia kuwa tunaabudu Mungu wa-kweli ambaye Yeye pekee anafahamu mambo yote kwa utimilifu; yaliyopita, yanayotendeka, na yatakayotokea, (ISA. 44:6-8).
Isitoshe, Mungu Baba katika Kisto Yesu ameipa Kanisa lake karama ya unabii, ili kuhami na mapema aila yake kabla hajatenda lolote. kwa kuwa kwanza huwajuza manabii zake alichoazimia kutenda nao hutueleza kuhusu makusudio ya Mola wetu, (UFU. 22: 6-7). Wala si hayo tu, Roho wa Mungu huchunguza yaliyomo moyoni mwa Mungu Baba na kuwajuza wateule zake, yaani, mimi na wewe ndugu katika Kristo. Sababu ikiwa kutuwezesha kuishi kwa utakatifu kama watu wa Mungu, ili tusifikwe na mambo kama watu wasio na ufahamu au hekima, (1KOR. 2:6-16).
Basi Wakristo, njia siyo nyingine ila, ile ile, walioipitia ndugu zetu walio tutangulia akina; Musa, Yusufu, Daudi, Danieli, Ezra, Petro, Mathayo, Yohana, Paulo, na juu ya wote Bw. Yesu, Mwokozi na Mkombozi wetu sote. Yeye alituonesha kwa matendo mfano uliobora zaidi ya wote. Na mfano huu ndio desturi ya Mwili wake (Kanisa) kote kote duniani na katika historia na tamaduni za watakatifu wa Mungu. Desturi na tamaduni hii sio nyengine ila kuomba bila kukoma na kuenda katika utakatifu tukimtumainia Mungu kwa imani, daima.
Tukitimiza haya sawa na ndugu zetu kabla yetu, Mungu atatuzidishia karama zote za rohoni na kamwe hatutapungukiwa kwa lolote. Utiifu wetu kwa Neno Takatifu na kwa dua zetu mbele zake, hizi ndizo zana walizotumia wenzetu kabla yetu kwa mafanikio makuu na ndizo baado tunazohitaji katika kipindi hiki kilichojaa giza na maovu ya kila aina. Tusikate tamaa wapenzi wa Mungu maana Mungu ni upendo na hakuna ajuae kupenda zaidi yake, wala hakuna aliye na uwezo wakupigania wapenzi wake zaidi yake Mwenyezi, Bwana wa Majeshi, (ISA. 41:1-16).
Tuseme nini zaidi wapenzi wa Mungu? Mie sioni lingine ila kijibidiisha katika Kulijua Neno Takatifu na kulitenda. Sawa na ushauri wa Mtume Paulo (1THES. 5:1-11), tukilijua Neno Takatifu tusilale usingizi kama wengine, bali tujivike kifuani imani na upendo na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu. Kwa kuwa Mungu hakutuweka kwa hasira yake, bali tupate wokovu kwa Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye alikufa kwa ajili yetu ili tuishi pamoja naye. Je, mwaona jinsi Mungu Baba alivyotufanya wandani wake? Basi tusijipunguzie karama iwayo yoyote ile. Tuzidi kutia bidii katika kumlingania Mungu Baba na kulisoma Neno Takatifu, maana, katika haya atatufunulia yote aliyotabiri kwa vinywa vya watakatifu wake na kutuandikia katika Biblia Takatifu.
Subscribe to:
Posts (Atom)